Featured Kitaifa

WAZIRI MAKAMBA ASHIRIKI MKUTANO WA 45 WA KAWAIDA WA BARAZA LA MAWAZIRI WA EAC

Written by mzalendo
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) akichangia hoja wakati wa Mkutano wa 45 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika tarehe 28 Juni, 2024 jijini Arusha.
Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki – anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato (Mb.) na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe. Stanslaus Nyongo (Mb.) wakifuatilia Mkutano wa 45 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa EAC uliofanyika tarehe 28 Julai, 2024 jijini Arusha.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (kati) akifatilia Mkutano wa 45 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa EAC pamoja na Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki – anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato (kushoto) na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki – anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi.
Kushoto ni Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Afrika Mashariki na Waziri wa Nchi anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki wa Jamhuri ya Sudan Kusini, Mhe. Deng Alor Kuol (kushoto) pamoja na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Veronica Mueni Nduva  wakiongoza Mkutano wa 45 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa EAC uliofanyika tarehe 28 Juni, 2024 jijini Arusha.
………

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) ameongoza ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Mkutano wa Kawaida wa 45 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) unaofanyika leo tarehe 28 Juni, 2024 jijini Arusha.

Mkutano huu pamoja na masuala mengine unapitia na kujadili masuala mbalimbali ya kipaumbele katika ukanda wa EAC ambayo ni, Maendeleo ya Miundombinu, forodha na biashara, masuala ya siasa na kijamii, taarifa ya kamati ya rasilimali watu pamoja na kupokea taarifa ya kamati ya ukaguzi na udhibiti wa hesabu za jumuiya kwa kipindi cha mwaka wa fedha unaoishia
Juni 2023.

Masuala mengine ni pamoja na, jitihada za kubidhaisha Kiswahili kikanda na kimataifa sambamba na taarifa ya Maadhimisho ya
Siku ya Kiswahili Duniani tarehe 7Julai ambayo kikanda yatafanyika nchini Kenya na kuhudhuriwa na Nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kadhalika, mkutano huu pia umejadili na kusisitiza umuhimu wa kuwasilisha michango ya mwaka kwa wakati kutoka kwa nchi zote
wanachama ili kuiwezesha Sekretarieti ya EAC kujiendesha na kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake ya kikanda.

Aidha, kupitia mkutano huo Katibu Mkuu Mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Veronica Mueni Nduva alijitambulisha kwa
Baraza hilo na kueleza nia yake ya kusimamia ustawi wa kikanda katika kukuza uchumi, uvumbuzi, biashara, ajira na amani na usalama kwa maendeleo endelevu ya wananchi wa EAC.

Viongozi wengine wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na, Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki – anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato (Mb.), Naibu Waziri, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe. Stanslaus Nyongo (Mb.), Makatibu Wakuu nMaafisa Waandamizi kutoka Wizara, Idara na Taasisi za Serikali.

Mkutano huo umefanyika chini ya Uenyekiti wa Jamhuri ya Sudan Kusini na umehudhuriwa na Nchi zote Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, isipokuwa Somalia imeshiriki kwa njia ya mtandao.

About the author

mzalendo