Featured Kitaifa

WAKUU WA MIKOA NA WASAIDIZI WENU ONGEZENI KASI YA KUSIKILIZA NA KUTATUA KERO ZA WANANCHI – MCHENGERWA

Written by mzalendo


Na Gideon Gregory Dodoma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mohamed Mchengerwa amewasisitiza wakuu wa mikoa na wasaidizi wao chini kuongeza kasi ya usikilizwaji wa kero za wananchi na kuzitatua pamoja na kuhusianisha programu ya Uimarishaji wa Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na kasi ya maendeleo katika maeneo yao.

Waziri Mchengerwa ametoa msisitizo huo leo Juni 27,2024 Jijini Dodoma wakati akizindua programu ya Uimarishaji wa Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuongeza kuwa wanapaswa kuongeze jitihada za kusikiliza kero za wananchi na kuzimaliza kwakushuka kwenye vijiji, mitaa mpaka Vitongoji.

“Ili ile dhamira ya kuleta programu hii, dhamira ya fedha inayotolewa Bilioni 200 ni fedha nyingi tunataka majibu ya fedha hizi kama ambavyo Mheshimiwa Rais amekusudia, niwaombe wakuu wa mikoa na niwaagize nendeni mkaongeze kasi ya utatuzi wa kero na ndio dhamira ya Rais anataka kuona kasi si ya kutatua kero peke yake lakini kuona namna ambavyo mnahusisha utolewaji wa huduma na kero husika ambazo zimewafikia katika maeneo yenu hili ni jambo la msingi ambalo sisi ofisi ya Rais TAMISEMI ni lazima tuongeze kasi ya utolewaji wa huduma kwa wananchi”,amesema.

Pia Waziri Mchengerwa amewaagiza Makatibu Tawala wa Mikoa kuongeza kasi ya utendaji ili fedha zilizotolewa kwenye programu hiyo ziweze kufanya kazi ambayo wataweza kuzielezea na kuwahasa kuwa wasikae maofisini bali wakatatue kero za wananchi.

Aidha ameongeza kuwa Licha ya mafanikio yaliyopatikana kupitia programu za Maboresho ya Serikali za mitaa tathmini mbalimbali zimebaini kuwepo kwa changamoto zikiwemo muingiliano wa majukumu katika utoaji wa huduma za kiuchumi na kijamii baina ya Wizara za kisekta na mamlaka za serikali za mitaa inayotokana na kukosekana kwa mfumo wa kisera na kisheria.

“Katika kukabiliana na changamoto hizo Serikali iliamua kuandaa programu ya Uimarishaji wa mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ambayo imeahinisha malengo yatakayotekelezwa ili kuwezesha mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza mipango inayohusu maendeleo na hivyo kukuza uchumi wa wananchi na kupunguza umaskini”, amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge TAMISEMI Denis Londo amesema programu hiyo itaenda kutatua changamoto kati ya serikali kuu na Serikali za Mitaa na kuibua vyanzo vipya vya mapato.

“Kamati inashauri kwamba uweponwa taasisi za utafiti ikiwemo mikoa ambayo ni mshirika mkubwa katika ukusanyaji wa maoni iendelee kushiriki hasa katika kuendeleza programu hii kwa kufanyia tadhmini utekelezaji wake”, amesema.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa wakuu wa mikoa Anthony Mtaka amesema kuwa wataenda kuhakikisha yale malengo ya Mhe.Rais ya kuona matokeo ya usimamiaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ngazi ya mikoa wanasimami yanakwenda vizuri.

About the author

mzalendo