Na Gideon Gregory, Dodoma.
Benki Kuu ya Tanzania kwa sasa inaendelea na hatua ya utafiti wa uanzishwaji wa matumizi ya Sarafu za Kidijitali za Benki Kuu (Central Bank Digital Currency).
Hayo yameelezwa leo Juni 27,2024 Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande wakati akijibu swali la Mbunge wa Kigamboni Mhe. Faustine Ndugulile aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuanza kwa matumizi ya Sarafu za Kidijitali (Central Bank Digital Currency) hapa nchini.
Amesema Benki Kuu imebaini kwamba, kama ilivyo kwa mataifa mengi, uanzishwaji wa Sarafu za Kidijitali za Benk Kuu (Central Bank Digital Currency), unahitaji kuanzishwa kwa uangalifu na umakini bila kuleta athari hasi katika mifumo ya malipo iliyopo nchini na pia kuweza kutatua tatizo halisi la malipo amabapo kwa sasa bado mifumo iliyopo nchini inakidhi hali halisi ya uwezeshaji mwananchi kutuma fedha na kufanya malipo.
“Aidha, soko letu bado linahitaji kuendelea kuboreshwa katika kuimarisha mifumo iliyopo kwa kutumia vyanzo vinavyopatikana kwa urahisi na wananchi wengi (simu za kawaida) tofauti na matumizi ya Sarafu za Kidijitali zinazoitaji matumizi ya simu janja (smartphones)”,amesema.
Ameongeza kuwa nchi nyingi ikiwa ni pamoja na majirani zetu na ukanda wetu bado wapo katika hatua hizo za awali za utafiti na kuboresha mifumo ya malipo iliyopo.