Featured Kitaifa

UBUNIFU WA MWANAFUNZI WAMSHAWISHI MSONDE KUMHAMISHIA SHULE MAALUM YA UFUNDI

Written by mzalendo

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – TAMISEMI (Elimu) Dkt. Charles Msonde amemuelekeza Ofisa Elimu mkoa wa Mara kushughulikia uhamisho wa Baraka Nyamuhanga mwanafunzji wa kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari Nimrod Mkono ili kuhamia shule ya Sekondari ya Ufundi Musoma baada ya mwanafunzi kuonesha ubunifu unaohitaji kuendelezwa.

Dkt. Msonde ametoa maelekezo hayo katika kikao kazi cha Walimu,walimu Wakuu,Wakuu wa Shule,Maofisa Elimu wa kata na Wilaya pamoja na Wasimamizi wa Elimu katika Wilaya ya Butiama mkoa wa Mara.

“Amenifurahisha sana mtoto baraka kwa kutengeneza shule yake na ameijenga mwenyewe kwa kuweka maumbo mbalimbali ya shule kwa kujenga majengo yote, picha zile zimenifurahisha sana lakini Baraka mwenyewe ameeleza namna anavyopenda ufundi kwasababu hiyo nimemwagiza Ofisa Elimu wa mkoa ahakikishe Baraka tarehe 01,Julai,2024 shule zinapofunguliwa ahamishwe kutoka shule yake ya kutwa apelekwe shule ya Sekondari ya Ufundi ya Musoma ili awe kwenye mkondo wa AMALI”

Dkt. Msonde anaendelea na ziara katika Halmashauri za mkoa wa Mara na kuwa na kikao kazi na Walimu,Walimu Wakuu,Wakuu wa Shule na Maofisa Elimu wa Kata,Wilaya,wadhibiti ubora,maofisa kutoka tume ya Utumishi wa Walimu na viongozi wa Chama cha Walimu wa Halmashauri hizo.

About the author

mzalendo