Featured Kitaifa

SERIKALI- ZOEZI LA UHAMAJI NGORONGORO LINALENGA KUWAPA WATU MAISHA BORA

Written by mzalendo

Na Sixmund Begashe

SERIKALI imesema zoezi linaloendelea la kuhama kwa hiari kutoka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro linalenga kuimarisha uhifadhi na kuboresha maisha ya watu.

Hayo yamesemwa mkoani Iringa na Msemaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii, John Mapepele wakati akiongea na waandishi wa habari ambao walitembelea kujionea ujenzi unaoendelea wa kituo cha kutangaza utalii nyanda za juu kusini chini ya mradi wa Kuboresha Utalii wa Kusini mwa Tanzania (REGROW) unaofadhiliwa na benki ya dunia.

Mapepele amesema kuwa serikali imeweka utaratibu mzuri katika kuhakikisha wale ambao wanahama wanapata makazi bora lakini pia wanalipwa fidia. Amesema zoezi hilo linazingatia haki za binadamu na kwamba uhamaji hufanyika baada ya malipo ya fidia kukamilika; kuvunja makazi au maendelezo na kuchagua mali wanazotaka kuhama nazo.

“Usafirishaji wa watu huanza baada ya michakato yote kukamilika. Wananchi wanaohama husafirishwa pamoja na mali zao ikiwemo mifugo; wanapata huduma zote safarini hadi Msomera au popote pengine wanapopachagua kuhamia,” amesema Mapepele.

Amefafanua kwamba, kwa wanaohamia maeneo mengine katika mikoa mbalimbali nchini, mbali ya usafiri wa kuhamia hulipwa pia shilingi milioni 15 za ziada kwa kila kaya badala ya shilini milioni 10.

Kwa wananchi wanaohamia sasa Msomera na baadaye itakuwa Kitwai na Saunyi, maandalizi huenda sambamba na uandaaji wa hati za nyumba ya vyumba vitatu iliyo katika eneo lenye ukubwa wa ekari 2.5 na shamba binafsi la ekari tano. Hati. Hizi hukabidhiwa wakuu wa kaya wakati wa kuagwa wakiwa bado Ngorongoro chini ya usimamizi wa Mkuu wa Wilaya.

Ameongeza kuwa Wananchi wanaohamia Msomera hupewa chakula magunia mawili ya mahindi kwa kila miezi mitatu kwa kaya kwa muda wa kipindi cha miezi 18 wakati wakiandaa mashamba;malisho,majosho na maji ya mifugo yao; kujengewa shule za msingi na sekondari,vivutio vya afya,mnada wa kisasa na vituo vya kuuzia maziwa;miundombinu ya maji,barabara,umeme,posta na mawasiliano;huduma za usalama na uangalizi wa Serikali kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni.

About the author

mzalendo