Featured Kitaifa

WAZIRI KAIRUKI ATOA WITO KWA NCHI WANACHAMA WA AFR100 KUWEKA MIFUMO YA UFUATILIAJI KATIKA KUONGOA MISITU ILIYOHARIBIWA

Written by mzalendo

Na Happiness Shayo

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) ametoa wito kwa nchi wanachama wa Mkakati wa Kuongoa Ardhi na Misitu iliyoharibiwa takribani Hekta milioni 100 Barani Afrika (African Forest Restoration Initiatives – AFR100), kuweka mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ya kielektroniki kuhakikisha lengo la kuongoa misitu hiyo linafikiwa kwa kuona uhalisia wa utekelezaji wa mkakati wa kuongoa misitu iliyoharibiwa.

Ameyasema hayo leo Juni 21,2024 jijini Dar es Salaam katika Mkutano wa 8 wa Mwaka wa nchi 34 za Afrika Wanachama katika Mkakati wa Uongoaji wa Ardhi na Misitu iliyoharibika.

“Naomba kupendekeza kwamba ni muhimu kuweka mifumo wa ufuatiliaji na urejeshaji wa misitu na mifumo ya uwajibikaji ili tuweze kuona hali halisi ya kinachoripotiwa katika maeneo husika kuhusu urejeshaji wa misitu” Mhe. Kairuki amesisitiza na kuongeza kwamba Tanzania imeanza kuangalia namna ya kuweka mfumo hiyo ili kuweza kufuatilia, kurahisisha upatikanaji wa taarifa.

Ameongeza kuwa katika kutekeleza mpango huo wa kurejesha misitu, Tanzania imefanikiwa kurejesha hekta milioni 2.4 kupitia afua za upandaji miti, ambayo ni sawa na asilimia 46.3 ambapo iliahidi kurejesha hekta milioni 5.2 za misitu na mandhari kwa mwaka 2018.

“Ili kudhihirisha nia thabiti ya Serikali ya utekelezaji wa mkakati wa kuongoa misitu nchini, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliongoza kampeni ya upandaji miti katika siku yake ya kuzaliwa mwaka 2023 kijijini kwao Kizimkazi Zanzibar ambapo zaidi ya miti 1,500 ilipandwa katika siku hiyo, lakini kampeni ya upandaji miti iliendelea kwa mwezi mzima ambapo miti takribani milioni 8.3 ilipandwa” Mhe. Kairuki aliweka bayana.

Amesema kuwa Rais Samia amekuwa kinara Barani Afrika na duniani katika kuhakikisha misitu inaongolewa na kutunzwa hasa kupitia kampeni yake ya nishati safi ambapo ameendelea kuhamasisha nchi nyingine duniani kutoa ahadi za kuhakikisha zinalinda misitu na zinaweka afua mbalimbali za kulinda misitu.

Mkutano huo umehudhuriwa na wawakilishi kutoka zaidi ya Nchi 34 Wanachama wa Afrika na Taasisi za Kifedha wanaojishughulisha na AFR100. Mkakati huo ulianzishwa Desemba 2015 ili kushughulikia changamoto za kimazingira, kiuchumi na kijamii zinazoathiri usimamizi wa maliasili Barani Afrika kwa lengo la kurejesha zaidi ya hekta milioni 100 za misitu iliyokatwa na kuharibiwa ifikapo mwaka 2030.

About the author

mzalendo