Na Mwandishi Wetu ,Tabora.
Mkoa wa Tabora umepokea Fedha za dharura kiasi cha shilingi milioni 790.541 kwaajili ya kurejesha mawasiliano ya miundombinu katika wilaya zake ambayo imeathiriwa na mvua za Elnino.
Hayo yameelezwa na Meneja wa Mkoa wa Tabora Mhandisi Lusako Kilembe wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Miundombinu OR-TAMISEMI Mhandisi Rogatus Mativila.
Mhandisi Kilembe amesema kwamba fedha hizo zitatumika kurejesha mawasiliano ya Barabara ambazo zilikatika kutokana na mvua hizo ili wananchi waweze kuendelea na shughuli zao za kawaida.
“Sasa hivi tumeanza kurejesha mawasiliano ya miundombinu katika Manispaa ya Tabora, pia wilayani kazi hizo zinaenda kuanza hivyo wananchi wataweza kupata huduma za kijamii ambapo awali wananchi hawakuweza kufanya shughuli hizo kwani mawasiliano yalikatika kabisa”.
Aidha, Mhandisi Kilembe alitaja fedha hizo za dharura zimepelekwa katika wilaya zote ambapo katika barabara ya Igunga-Itumba-Simbo milioni 100(Igunga), milioni 73.766 barabara ya Kazaroho-Mpandamlowoka (Kaliua), barabara ya Mwangoye-Senge-Nindo-Mwamala milioni 92 (Nzega),barabara ya Kitangili-Mbogwe-Nhele milioni 64.8 (Nzenga TC) barabara ya Usunga-Imalampaka na Urafiki-Mwanasongezya milioni 57 (Sikonge) na barabara ya Ndeyelwa na Kakola-Ikomwa na Igombe-Igambilo milioni 275( Manispaa ya Tabora).
Amesema fedha hizo zitatumika kufukia mashimo kwa kujaza vifusi, ujenzi wa Kalvati, kunyanyua tuta za barabara, kuweka changarawe, kurekebisha kingo za maji, ujenzi wa boksi kalvati, kuimarisha kingo za madaraja pamoja na kuondoa maji kwenye mitaro ya barabara.
Hata hivyo Meneja huyo amewataka wananchi wa mkoa wa Tabora kutunza miundombinu kwani fedha nyingi zinatumika kujenga barabara hivyo wanapaswa kulinda miundombinu ili kusitokee watu watakaoharibu kingo za barabara pamoja na alama zake na endapo itatokea hivyo ni vyema wakatoa taarifa kwenye mamlaka za serikali.
“Nitoe rai kwa wananchi waweza kulinda miundombinu hii kwakuwa wapo baadhi ya watu wana tabia ya kukata bomba na vifaa vingine kwenye kingo za madaraja pamoja na alama za barabarani,watambue kwamba serikali inatumia fedha nyingi kurejesha miundombinu hiyo na wao kama watumiaji wa barabara hizo wanapaswa kuzilinda ili ziweze kutumika kwa muda mrefu.
Mkoa wa Tabora una hudumia mtandao wa Barabara wa urefu wa km. 8,404.88 kati ya hizo km.112 za lami, km. 620 barabara za udongo, km. 2007 za barabara za changarawe.
Naye, Mtendaji wa kijiji cha Magoweko Bw. Onesmo Halinga amesema wanaishukuru sana serikali chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia fedha na hivyo kurejesha mawasiliano ambayo kipindi cha masika barabara zilikatika.
Amesema mvua hizo zilisababisha gharama za usafiri kupanda ila kwa sasa mawasiliano yamerudi na wanaendelea na shughuli zao za kawaida na pia wanaishukuru TARURA kwa usimamizi wao mzuri kwani sasa hivi barabara zinapitika.