Featured Kitaifa

VIHATARISHI VYA BAJETI VYATAJWA

Written by mzalendo

Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba amesema utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/25 unaweza kuathiriwa na vihatarishi mbalimbali vinavyohusisha mabadiliko ya sera za uchumi, fedha, bajeti, siasa na mahusiano ya kidiplomasia.

Dkt. Nchemba ameyasema hayo leo Juni 13,2024 Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa mwaka 2024/25 na kuongeza kuwa utekelezaji wa bajeti unaweza kuathiriwa na masuala mtambuka hususani mabadiliko ya tabianchi, majanga ya asili, magonjwa ya mlipuko na athari za vita baina ya mataifa.

“Vihatarishi katika bajeti ya mwaka 2024/25 ni pamoja na kudorora kwa uchumi wa dunia, mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma, mabadiliko ya riba katika masoko ya fedha ndani na nje ya nchi, mabadiliko ya viwango vya kubadilisha fedha, madeni sanjari siasa na mahusiano ya kidiplomasia, na mabadiliko ya tabianchi, majanga ya asili na magonjwa ya mlipuko.

Amesema endapo vihatarishi hivyo vitatokea, athari zinazoweza kujitokeza ni pamoja na kutokufikiwa kwa lengo la ukusanyaji wa mapato, kasi ndogo ya utekelezaji wa miradi, kuongezeka kwa gharama za bidhaa, malighafi, huduma na utekelezaji wa miradi, kuongezeka kwa gharama za kuhudumia deni la Serikali na kuongezeka kwa gharama za mikopo ya kibiashara katika masoko ya fedha.

About the author

mzalendo