WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa umma nchini kote wawatumikie wananchi ipasavyo na wahakikishe wanaondoa urasimu kwa kutowasumbua wananchi wanaokuja kupata huduma za kiserikali katika ofisi zao.
“Epukeni tabia ya kuomba na kupokea rushwa, rushwa inaharibu maendeleo. Tusitumie maneno magumu kwa wananchi wetu maana eneo hili bado ni changamoto, tunalishughulikia au bado tupo kwenye mchakato, tunafanya tathmini, upembuzi yakinifu, tumieni lugha rahisi.“
Pia, Waziri Mkuu amewataka watumishi hao wazingatie taaluma zao na watoe ushauri kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma, wafike sehemu ya kazi kwa muda uliopangwa na watumie muda huo kufanya kazi za Serikali na waepuke kuwa na migongano ya maslahi katika kutekeleza majukumu na kusimamia rasilimali za umma.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Juni 12, 2024) kwenye Mkutano Mkuu wa 14 wa Taasisi ya Maboresho ya Serikali za Mitaa Tanzania (TOA) unaofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) jijini Arusha.
“Viongozi wote tuwahudumie wananchi kwa heshima, staha, unyenyekevu na umakini mkubwa ikiwa ni pamoja na kuwapa majibu sahihi ya maswali yao na majawabu sahihi ya kero zinazowasumbua. Toeni ufafanuzi au maelekezo juu ya masuala yatokanayo na sheria, kanuni na taratibu za Serikali kwa haraka, uwazi na bila upendeleo wowote au ubaguzi wa aina yoyote.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuhakikisha wananchi wote wanapata maendeleo na huduma mbalimbali za msingi.
Amesema chombo muhimu cha kuhakikisha maendeleo yanafika kwa wananchi wa ngazi ya msingi ni Mamlaka za Serikali za Mitaa na maendeleo hayo yatakuwa dhahiri na endelevu endapo wananchi watashirikishwa katika kuainisha changamoto zinazowakabili na watawezeshwa kukabiliana nazo kwa kutumia rasilimali zinazowazunguka.
Pia, Waziri Mkuu amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri wahakikishe wanakuwa na mifumo madhubuti ya ukusanyaji na usimamizi wa mapato pamoja na kuweka mkakati wa udhibiti wa mali zilizopo ndani ya halmashauri na mapato watakayoyapata wayaelekeze katika kukamilisha miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika halmashauri zao.