Featured Kitaifa

WAAMBIENI WANANCHI MADHARA YA KUCHAGUA VIONGOZI WANAOTOA RUSHWA -MHE.SIMBACHAWENE 

Written by mzalendoeditor

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza na Viongozi wa TAKUKURU (hawapo pichani) wakati akifungua kikao kazi cha viongozi hao kilichofanyika Kibaha mkoani Pwani katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere.

Sehemu ya Viongozi wa TAKUKURU wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) wakati akizungumza nao kabla ya Waziri huyo kufungua kikao kazi cha Wakuu wa TAKUKURU Mikoa, Naibu wa TAKUKURU Mikoa, Wakuu wa TAKUKURU Wilaya na Wakuu wa TAKUKURU vituo maalumu kilichofanyika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere mkoani Pwani.

Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi, Salum Hamduni akielezea lengo la kikao kazi cha Wakuu wa TAKUKURU Mikoa, Naibu wa TAKUKURU Mikoa, Wakuu wa TAKUKURU Wilaya na Wakuu wa TAKUKURU vituo maalumu kilichofanyika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere mkoani Pwani kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kuzungumza na viongozi hao.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bi. Neema Mwakalyelye akitoa utambulisho wa viongozi waliohudhuria kikao kazi cha Wakuu wa TAKUKURU Mikoa, Naibu wa TAKUKURU Mikoa, Wakuu wa TAKUKURU Wilaya na Wakuu wa TAKUKURU vituo maalumu kilichofanyika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere mkoani Pwani.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akisalimiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Pwani mara baada ya kuwasili katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere kwa lengo la kufungua kikao kazi cha Wakuu wa TAKUKURU Mikoa, Naibu wa TAKUKURU Mikoa, Wakuu wa TAKUKURU Wilaya na Wakuu wa TAKUKURU vituo maalumu.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akifurahia jambo na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi, Salum Hamduni (kushoto) mara baada ya Waziri Simbachawene kupokea zawadi ya tai yenye nembo ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wakati wa kikao kazi cha viongozi wa TAKUKURU kilichofanyika Kibaha mkoani Pwani katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya viongozi wa TAKUKURU baada ya kufungua kikao kazi cha viongozi hao kilichofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha mkoani Pwani. Kulia kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi, Salum Hamduni. Kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge.

Na. Veronica Mwafisi-Kibaha

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amewataka Viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kutumia taaluma na ujuzi waliokuwa nao katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya kupokea rushwa hasa katika kipindi cha uchaguzi wa viongozi mbalimbali.

Mhe. Simbachawene ametoa kauli hiyo leo tarehe 3 Juni, 2024 katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha mkoani Pwani wakati akifungua kikao kazi cha viongozi wa TAKUKURU kilicholenga kujiimarisha zaidi katika kuzuia na kupambana na rushwa wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa, na Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.

Mhe. Simbachawene amesema ni wakati sasa wa wananchi kupewa elimu kwa nguvu zote juu ya rushwa katika uchaguzi ili kupata viongozi bora kwa maendeleo ya taifa kwani kundi kubwa la wananchi linaamini kuwa mtu hawezi kumchagua kiongozi anayemtaka mpaka apewe rushwa. 

“Kuzuia wananotaka kutoa rushwa pekee hakutoshi kwani makundi ya wapiga kura wanasadiki kuwa mtu hawezi kumchagua kiongozi anayemtaka mpaka awe amepewa chochote, hivyo tuwaelimishe na tuyaishi maisha ya kwenye vitabu vya dini kuwa anayetoa na anayepokea rushwa, wote wana hatia,” Mhe. Simbachawene amesisitiza.

Amesema sote tunatambua kwamba uchaguzi wa viongozi ni jambo muhimu kwa mtu mmoja mmoja na kwa Taifa kwa ujumla kwa sababu uchaguzi unagusa moja kwa moja maisha ya wananchi wetu na mustakabali wa maendeleo ya Taifa letu.

Ameongeza kuwa vitendo vya rushwa na makosa mengine yanayofanyika kabla au wakati wa kuchagua viongozi, yanaharibu mchakato wa uchaguzi na huwapoka baadhi ya wapiga kura haki ya kumchagua mgombea wanayemtaka. 

Na kuongeza kuwa, vitendo hivyo huwanyima haki baadhi ya wagombea kushiriki au kushindana kwa usawa katika uchaguzi huo. “Madhara ya uwepo wa vitendo hivi ni pamoja na kupatikana viongozi wasiokuwa waadilifu na kuchelewa kupatikana au kutopatikana kabisa kwa maendeleo na ustawi wa jamii ya Watanzania, kinyume na matamanio ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hivyo, hatuna budi kuweka mikakati madhubuti ya kuzuia vitendo hivyo kuanzia hatua za awali kabisa za mchakato wa uchaguzi” Mhe. Simbachawene amesema.

Akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha Mhe. Simbachawene kufungua kikao kazi hicho, Mkurugenzi wa TAKUKURU, CP Salum Hamduni amesema kikao kazi hicho cha siku tatu kwa viongozi hao wa TAKUKURU kimelenga kujipanga katika Kuzuia na Kupambana na Rushwa wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.

CP Hamduni ameongeza kuwa ni wakati sasa wagombea na wananchi kufahamu madhara ya rushwa katika uchaguzi na kuongeza kuwa watajipanga vema na kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa ufanisi mkubwa bila ya kuwa na chembechembe za rushwa hatimaye kuwapata viongozi bora kwa maendeleo ya taifa kama ilivyokusudiwa na serikali.

 

About the author

mzalendoeditor