Mbunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), Zohreh Elahian amekuwa mwanamke wa kwanza kujiandikisha kugombea uchaguzi wa mapema wa duru ya 14 ya urais wa Jamhuri ya Kiislamu, kufuatia kifo cha Rais Ebrahim Raisi katika ajali ya helikopta.
Msemaji wa Makao Makuu ya Uchaguzi ya Iran Mohsen Eslami, amesema watu 23 walifika katika ofisi zao zilizoko katika Wizara ya Mambo ya Ndani kwa ajili ya kujiandikisha kuwania nafasi ya urais jana Jumamosi, lakini wanane tu ndio waliopitishwa.
Mbali na mwanamama huyo, wengine walioidhinishwa kugombea kiti cha rais nchini humo ni pamoja na Mbunge wa jiji la Tabriz, Masoud Pezeshkian, na Vahid Haghanian, msaidizi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na ambaye pia amewahi kuwa Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).
Wengine waliodhinishwa jana kugombea kiti cha urais katika uchaguzi wa mapema wa urais ni Meya wa jiji la Tehran, Alireza Zakani, Mbunge wa zamani, Sayyid Ahmad Rasoulinejad na wanasiasa Alireza Zakani, Sayyid Ahmad Rasoulinejad, Habibollah Dahmardeh, na Sayyid Mohammad-Reza Mirtajodini.
Hadi sasa idadi ya watu waliojiandikisha kugombea kiti cha urais nchini Iran imeongezeka hadi kufikia 17 baada ya wengine Nane zaidi kujiandikisha kuwania nafasi hiyo jana Jumamosi. Usajili wa wagombea wa urais ulianza Alkhaisi na unatazamiwa kumalizika kesho Jumatatu.
Uchaguzi wa mapema wa duru ya 14 ya urais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umepangwa kufanyika Ijumaa ya tarehe 28 Juni baada ya kifo cha Rais Sayyid Ebrahim Raisi katika ajali ya helikopta mnamo mwezi Mei 19 mwaka huu.
Watu wote waliojiandikisha kuwania urais, sharti waidhinishwe na Baraza la Walinzi wa Katiba la Iran lenye wanachama 12, jopo ambalo hukagua sifa za wenye azma ya kugombea nafasi hiyo, mbali na kusimamia zoezi zima la uchaguzi.