Featured Kitaifa

TBS KANDA YA KATI YATEKETEZA BIDHAA ZISIZO NA UBORA

Written by mzalendoeditor

 

Afisa Mdhibiti ubora Kanda ya kati TBS, Sileja Lushibika, akizungumza na waandishi habari leo Mei 31,2024 jijini Dodoma mara baada ya kuteketeza vyakula pamoja na vipondozi vyenye thamani ya shilingi milioni 42.5.

Afisa Mdhibiti ubora Dodoma TBS Bi. Halima Msonga,akizungumza na waandishi habari leo Mei 31,2024 jijini Dodoma mara baada ya kuteketeza vyakula pamoja na vipondozi vyenye thamani ya shilingi milioni 42.5.

Na.Alex Sonna_, Dodoma.

Shirika la viwango nchini TBS limeteketeza vyakula Pamoja na vipodozi mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni 42.5 kutokana na kubaini zipo chini ya kiwango.

Akizungumza leo Mei 31,2024 Jijini Dodoma mara baada ya zoezi hilo, Afisa Mdhibiti ubora Kanda ya kati Sileja Lushibika amesema kuwa walifanya oparesheni ya Ukaguzi Kanda ya kati na kubaini kuwepo usanganyifu kwa baadhi ya wafanyabiashara kuuza bidhaa zilizopo chini ya kiwango.

“Bidhaa hizi tulizikamata kwenye oparesheni mbalimbali tunayoifanya sisi TBS kwasababu ni jukumu letu la kuhakikisha watanzania wanakuwa salama maana ndiyo wametupa dhamana ya kuwatumikia na wanakula chakula chenye kiwango”,amesema.

Ameongeza kuwa bidhaa hizo wamezikamata katika mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora.

Aidha amewaonya wanawake wanaotumia vipodozi kuwa makini navyo kwani kwasasa vingi vina sumu inayoweza kuharibu ngozi zao.

“Tunawaomba sana ndugu zetu wakina mama, dada zetu mwenyezi Mungu amewaumba kwa sura nzuri, hivyo hatuna budi kukubaliana nazo kwani hivi vipodozi vina madhara mengi mno”,ameongeza.

Pia amewaonya wafanyabiashara wanaouza bidhaa zilizoisha muda wake ambapo amesema wanapaswa kuwa na utamaduni wa kukagua bidhaa zao na kama zimeisha muda wake ni vyema wakaziondoa mara moja ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza.

Kwa upande Wake Afisa Mdhibiti ubora Dodoma Halima Msonga ametoa wito kwa wafanyabiashara na Wananchi huku akisistiza kuwa zoezi hilo ni endelevu.

“Rai yangu kwa watanzania, kwa wamama na ndugu zangu wengine tuwe makini na vitu tunavyo nunua dukani, ikiwezekana kama ni bidhaa iliyozalishwa Tanzania inapaswa kuandikwa kwa lugha ya Kiswahili lakini kama inatokea nje inapaswa kuandikwa kwa lugha mbili kama ni Kingeleza basi na Kiswahili kiwepo”,amesema.

About the author

mzalendoeditor