Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI anayeshughulikia Afya Mhe. Dkt. Festo Dugange (Mb) amesema, Serikali inatarajia kuajiri watumishi wa kada za walimu 12,000 ambapo baadhi yao watapangiwa katika maeneo yenye upungufu mkubwa zaidi zikiwemo Shule za tarafa za Mwembe – Mbaga, Same na Chome – Suji.
Dkt.Dugange amesema hayo Bungeni Jijini Dodoma katika kipindi cha Maswali na Majibu wakati akijibu swali la Mheshimiwa David Mathayo David, Mbunge wa Jimbo la Same Magharibi aliyeuliza Je, Serikali ina mpango gani na Shule za Mwembe – Mbaga, Same na Chome – Suji ambazo hazina Walimu kutokana na mazingira magumu ya kazi?
“Serikali imekuwa ikiajiri walimu kila mwaka na kuwapangia vituo vya kazi kulingana na mahitaji ambapo maeneo yenye mazingira magumu hupewa kipaumbele. Kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2020/21 hadi 2022/23 Halmashauri ya Wilaya ya Same ilipangiwa walimu 364 wakiwemo walimu 249 wa shule za msingi na walimu 115 wa shule za sekondari.”
Aidha Mhe. Dkt Dugange amewaelekeza wa Wakurugenzi wote Nchini kutekeleza mpango wa kutoa motisha kwa Watumishi wanaoishi katika maeneo ya mbali au magumu ambayo hutengwa kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ili Watumishi waendelee kutoa huduma wakiwemo Walimu.