Featured Kitaifa

MUHULA WA KWANZA KIDATO CHA TANO KUANZA JULAI 1

Written by mzalendo

Na Gideon Gregory, Dodoma.

Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali ikiwemo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imekamilisha zoezi la Uchaguzi wa Wanafunzi wa Kujiunga na Kidato cha Tano katika Shule za Sekondari na Vyuo vya Elimu ya Ufundi vya Serikali kwa mwaka 2024 ambapo Wanafunzi waliochaguliwa ni kutoka Shule za Serikali, zisizo za Serikali na watahiniwa wa kujitegemea waliofanya mtihani chini ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima.

Taarifa hiyo imetolewa leo Mei 30,2024
Jijini Dodoma mbele ya waandishi wa Habari na
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mohamed Mchengerwa amesema muhula wa kwanza kwa wanafunzi wa Kidato cha Tano utaanza Julai 1 2024 hivyo, Wanafunzi wote waliopangwa kujiunga na Kidato cha Tano kwa mwaka mwaka huu wanapaswa kuanza kuripoti Shuleni kuanzia tarehe Juni 30.

“Uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo vya Elimu ya Ufundi umefanyika kwa kuzingatia ufaulu na nafasi zilizopo katika Shule; hivyo, hakutakuwa na fursa ya kufanya mabadiliko yoyote ya Shule kutokana na ukosefu wa nafasi”, amesema.

Aidha, ametoa wito kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa azma ya Serikali ya kuwa na Shule za Sekondari za Kidato cha Tano katika kila Tarafa inatekelezwa, ili kuwezesha wanafunzi wote wanaofaulu Mtihani wa Kidato cha Nne kupata nafasi ya kuendelea na masomo ya Kidato cha Tano na Sita.

“Upanuzi na ujenzi wa Shule Mpya za Kidato cha Tano na Sita uendelee kufanyika ikiwa ni pamoja na kuongeza tahasusi za masomo ya Sayansi, Mikoa ihakikishe inakuwa na tahasusi zote za msingi katika shule zake ili kuwapunguzia wazazi/walezi na wanafunzi gharama za usafiri kwenda shule za mbali”,amesema.

Pia ametumia fursa hiyo kuwapongeza walimu, wazazi na walezi wote kwa juhudi walizozifanya katika malezi na ufundishaji hali iliyowezesha wanafunzi kufaulu vizuri.

“Naomba wazazi/walezi wote tuendelee na moyo huu wa kusimamia na kufuatilia maendeleo ya watoto wetu ikiwemo kuwalea katika malezi na maadili mema ili wawe raia wema na wanaotegemewa na Taifa letu”, amesema.

Amewapongeza wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo vya Elimu ya Ufundi na kuwahimiza kuendelea kufanya bidii katika kujifunza ili waweze kufanikiwa kujiunga na mafunzo ya elimu ya juu baada ya kuhitimu Kidato cha Sita na Vyuo vya Elimu ya Ufundi.

Pamoja na pamoja na taarifa hiyo amesema pamoja na maelekezo haya, kwa mwanafunzi, mzazi/mlezi atakayekuwa na suala linalohitaji maelekezo au ufafanuzi zaidi aende katika Ofisi za Elimu za Mikoa na Halmashauri.

About the author

mzalendo