Na Ramadhani Kissimba na Farida Ramadhani, WF, Nairobi- Kenya
Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) imeahidi kuendeleza ushirikiano uliopo kati yake na Tanzania kwa kuendelea kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba katika kikao kati ya Tanzania na Benki ya Maendeleo Afrika Mashariki, kando ya Mikutano ya Mwaka 2024 ya Bodi ya Magavana (Mawaziri wa Fedha kutoka nchi wanachama) wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Jijini Nairobi nchini Kenya, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, alisema Tanzania ni mojawapo ya nchi zinazofaidika na uwepo wa Benki hiyo, kutokana na uhusiano mzuri uliopo kati ya pande hizo mbili.
Dkt. Mwamba alisema Benki hiyo imekuwa ikifadhili miradi mbalimbali nchini ikiwemo miradi ya taasisi za Serikali kama vile Shirika la Nyumba, benki za biashara kama Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB) na miradi inayotokana na sekta binafsi.
Aidha Dkt. Mwamba alisema sanjari na ufadhili wa miradi ya EADB kwa Tanzania Bara, pia mazungumzo yanaendelea kuhusu miradi mingine kwa upande wa Zanzibar hasa miradi ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu.
“Tunaendelea kuzungumza kuhusu miradi mingine, hususan Zanzibar ambapo tumezungumza kuhusu mradi wa ujenzi wa makazi ambao kwa sasa tutaufuatilia kwa karibu ili kuona unafanikiwa”, alisema Dkt. Mwamba.
Dkt. Mwamba aliongeza kuwa Benki hiyo imeonesha nia ya kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi ya maendeleo na kwa sasa Tanzania ina asilimia 73 za miradi ambayo inatekelezwa na Benki hiyo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil, alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeikaribisha Benki ya EADB kufanya mazungumzo yatakayosaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Maendeleo visiwani humo.
Dkt. Akili aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC) inatafuta ufadhili wa kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba takribani 3,000 za bei nafuu, hivyo Zanzibar inaona ni fursa kuitumia Benki hiyo kutekeleza mradi huo.
‘’Kuna Shirika la Nyumba Zanzibar ambalo kwa sasa linaendelea kutafuta wafadhili ili kutekeleza ujenzi wa nyumba za bei nafuu, hivyo tumewaalika Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki ili tuzungumze nao kuhusu utekelezaji wa ujenzi wa nyumba hizo” , alisema Dkt. Akili.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Bi. Viviene Yeda ametoa wito kwa Tanzania na nchi nyingine za Afrika Mashariki kuchangamkia fursa zinazopatikana katika Benki hiyo kutokana na uwiano uliopo katika umiliki wa hisa unatokana na Benki hiyo ambapo Tanzania, Kenya na Uganda zina hisa sawa.
Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) ni mshirika wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Standard Charter Bank ambayo inahudumia nchi wanachama sita (6) ikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudani Kusini.