Na WMJJWM, Njombe
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Madini Mhe. Dkt. Dotto Biteko amesema kumekuwa na mwitikio mkubwa kwa wanaume katika kutafuta msaada wa kisheria kuliko wanawake.
Ameyasema hayo wakati akizindua Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign), mkoani Njombe Mei 26, 2024.
Mhe. Biteko amesema tangu kuanza kwa kampeni hiyo wanaume waliojitokeza ni 416000 wakati wanawake ni 199000 ambapo amesema awali wanaume walikuwa wagumu kutumia huduma za ustawi wa jamii na kisheria kwenye kupambana na ukatili wa kijinsia, sasa mwitikio unaongezeka.
Ametoa wito kwa watoa huduma wa msaada wa kisheria kuwa na nia moja ya kutafuta suluhu miongoni mwa jamii badala ya kutafuta mshindi ni nani ili kuepuka roho za visasi na kuwa na jamii inayostahimiliana.
Aidha ametoa rai kwa wananchi wote kutumia fursa ya kupata msaada na elimu ya sheria mbalimbali wakati wowote bila kusubiri wapatapo shida.
“Na hili amelisema vizuri Waziri wa Maendeleo ya Jamii kuwa ni vema kutoa msaada mapema kabla ya migogoro, tukisubiri watu wameshagombana, watoa huduma wanakuja kushughulika na visasi badala ya elimu. Baba na mama wakigombana wanaokosa dira ni watoto lakini pia kuna wazee wanaowategemea wanakosa msaada matokeo yake wanakuwa mzigo kwa jamii” amesema Mhe. Biteko.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akitoa salaam za Wizara, amesema Kampeni ya Msaada wa kisheria ya Mama Samia Legal Aid Campaign ni muhimu kwa mustakabali wa kuimarisha ustawi na maendeleo ya jamii.
“Kampeni hii ni mkombozi wa makundi maalum, kwani wamekuwa wakihangaika kutafuta ustawi wao lakini wanaonewa wakati mwingine hawajui watapaje msaada ndio sababu Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliamua kuunda Wizara hii kushirikiana na Wizara nyingine, ili Maafisa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii wanyanyue ustawi ikiwemo msaada wa kisheria” amesema Waziri Gwajima.
Ameeleza kwamba, msaada wa kisheria utawezesha kutatua changamoto zinazoikabili jamii ikiwemo watoto, wanawake, wazee na wafanyabiashara ndogondogo wakiwemo Machinga, Mama/baba lishe na Bodaboda.
Aidha, Waziri Dkt. Gwajima amewaasa wanaume kuendelea kujitokeza na kusimama kwenye nafasi zao katika familia, halikadhalika na wanawake.