Na Mwandishi Wetu, Malinyi
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeanza utekelezaji wa agizo la Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa la kurekebisha haraka barabara zilizokatika wilayani Malinyi ili kurejesha huduma kwa wananchi.
Naibu Katibu Mkuu anayesimamia miundombinu OR-TAMISEMI, Mhandisi Rogatus Mativila amefika eneo lililoathiriwa na mvua na kuhimiza utekelezaji wa haraka ndani ya muda uliopangwa.
“Mhe. Waziri Mchengerwa alitembelea barabara na madaraja yaliyokatika kutokana na athari za mvua na kujionea barabara hii ya Lugala-Misegese ikiwa imekatika na kusababisha magari kutopita na akaelekeza mara moja barabara hii irekebishwe na mimi kama Naibu Katibu Mkuu ninayeshughulikia miundombinu nimefika nione hali ipoje na tunarekebishaje haraka kwani Waziri alitoa pia maelekezo kwamba fedha zitolewe, fedha zipo na mkandarasi apatikane kurekebisha eneo hili”.
Aidha, amesema moja ya barabara iliyopata changamoto ni barabara inayoenda kwenye hospitali ya wilaya kutokana na dharura hiyo imebidi wamchukue mkandarasi aliyepo jirani afike na aanze kufanya kazi na tayari mkandarasi huyo ameanza kupeleka vifaa kama alivyoagiza Mhe. Waziri kwa kutoa siku nne mkandarasi apatikane na aanze kazi kuhakikisha panapitika.
“Tunategemea ndani ya hizo siku nne alizopewa angalau wananchi waweze kupita kwa magari wakati marekebisho makubwa yanaendelea. Na mimi nimeliona hilo naenda kulisimamia haraka, wakituletea tu maombi ya fedha, fedha hizo tutazileta mkandarasi yupo hapa tayari kuanza kazi”, amesema.
Vile vile ameiagiza TARURA kusimamia kazi hiyo usiku na mchana ili ikamilike haraka na mkandarasi aweke wafanyakazi na vifaa vya kutosha.
Naye, Katibu Tawala Wilaya ya Malinyi, Bi. Saida Mhanga amesema barabara ya Malinyi – Igawa wanaitumia kuelekea ofisini na nyenzo kuu inayotumika hivi sasa ili waweze kufika kazini ni pikipiki. Hivyo amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea milioni 800 kwa ajili ya kurekebisha mawasiliano wilayani hapo.
Amesema kwa asilimia 95 ya chanzo kikubwa cha mapato wilaya ya Malinyi ni kilimo ikiwemo ufuta, mahindi, choroko na mengineyo hivyo kurejesha barabara hayo itawasaidia wakulima katika msimu huu wa mavuno.
Mhandisi Charles Mang’era Meneja TARURA Wilaya ya Malinyi amesema wilaya hiyo ni kati ya wilaya ambazo zimepata madhara makubwa kutokana na mvua za masika zilizoanza Novemba mwaka jana mpaka katikati ya Mei mwaka huu hivyo miongoni mwa madhara ambayo yamejitokeza katika wilaya yao ni miundombinu kukatika.
“Takriban Km. 53 za barabara zimepata madhara ya kukatika, miongoni mwa ambazo zimeathirika zaidi ni hii ya Malinyi – Igawa na Lugala –Misegese, Serikali imekuwa sikivu wametupatia Shilingi Mil. 800 fedha za dharura kuhakikisha barabara zote mbili zinafunguka na wananchi wanapata huduma”.
Wakati huo huo Mkurugenzi wa ufundi kutoka kampuni ya Bavaco Mellezier Limited Mhandisi Nkolate Ntije amesema tayari wameshapeleka vifaa muhimu kwaajili ya kuanza utekelezaji wa kurejesha mawasiliano ya barabara hizo na kuongeza kwamba wanaishukuru Serikali kwa kuwaamini na kuahidi kukamilisha kwa muda waliopewa.