Featured Kitaifa

TARURA TENGENI FEDHA ZA UJENZI WA BARABARA YA LAMI MIKUMI’

Written by mzalendo

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mohamed Mchengerwa ameutaka Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuweka kwenye bajeti ujenzi wa barabara ya lami katika eneo linalozunguka Kituo cha Afya Mikumi.

Waziri Mchengerwa ameyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa kituo cha Afya Mikumi wakati wa ziara yake mkoani Morogoro leo tarehe 20.05.2024.

Amesema kituo hicho ni muhimu kwa wakazi wa Mikumi na maeneo ya jirani.

“Tumesikia taarifa ya kituo hiki kuwa kinahudumia zaidi ya wananchi 31,000, lakini wakati wa masika hakifikiki kwa kuwa kinazingirwa na maji, hivyo TARURA nawalekeza kuweka mpango wa ujenzi wa barabara za lami kuzunguka kituo hiki ili wananchi waweze kufika wakati wote.”

Wakati huo huo, Mhe. Mchengerwa ameutaka uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kutenga bajeti kwenye mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa uzio na njia ya kutembelea (Walk way) ili wananchi wapate huduma bora na kuimairisha usalama wa kituo.

“Halmashauri yenu ina mapato ya kutosha na kazi kama hizi za ukamilishaji mmaweza kufanya kwa kutumia mapato ya ndani, hivyo tengeni fedha na mjenge uzio hapa na tumeona tope hili hapa kwa sababu ya mvua inakua ni vigumu wagonjwa kutoka jengo moja kwenda lingine hivyo mkajenga na njia za waenda kwa miguu,” amesisitiza Mchengerwa.

Naye Mbunge wa Jimbo la Mikumi, Mhe. Denis Londo ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kituo cha Afya Mikumi na kuomba kuongezewa fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo la kuhifadhia maiti na jengo la utawala.

About the author

mzalendo