Featured Kitaifa

MFUKO WA WCF WATAKIWA KUONGEZA WIGO WA WANACHAMA

Written by mzalendoeditor

Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe Mhe. Fatuma Toufiq (katikati) akieleza jambo wakati wa Kikao cha kuwajengea uelewa kuhusu masuala ya Fidia kwa Wafanyakazi, katika ofisi za WCF jijini Dodoma. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Hifadhi ya Jamii, Bw. Festo Fute.

Na; Mwandishi Wetu – Dodoma

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeutaka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) uliopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kuogeza jitihada ya kusajili wanachama wapya ili kuhakikisha nguvu kazi ya Taifa inalindwa na fidia inatolewa kwa wafanyakazi wanaopata ugonjwa au ajali inayotokana na kazi.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Fatuma Toufiq, wakati walipotembelea Makao Makuu ya Ofisi za WCF, jijini Dodoma kwa lengo la kupata uelewa wa masuala ya fidia kwa wafanyakazi.

Amesema kuwa, Sekta binafsi inakuwa kwa kasi na imeendelea kuleta tija katika kuchangia kodi na kutengeneza ajira zaidi, hivyo amesisitiza mfuko huo kuhakikisha unasajili waajiri wengi zaidi katika sekta hiyo.

Vile vile, ameipongeza WCF kwa kulipa fidia kwa wafanyakazi wanaostahili, pamoja na kuwa na utaratibu wa kutoa elimu kwa makundi mbalimbali kuhusu elimu ya fidia kwa wafanyakazi.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Riziki Lulida ametoa rai kwa waajiri kutambua wajibu wa kutoa michango kwa ajili ya wafanyakazi wao ili ikitokea madhila yatokanayo na kazi mfuko huo wa WCF uweze kutoa fidia.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Dkt. John Mduma ameahidi kufanyia kazi maoni ya kamati huku akieleza kuwa WCF imejipanga kusajili wanachama wengi zaidi kwa kuimarisha mifumo ya kutolea huduma ambayo itawawezesha Waajiri wengi zaidi kujisajili.

Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe Mhe. Fatuma Toufiq (katikati) akieleza jambo wakati wa Kikao cha kuwajengea uelewa kuhusu masuala ya Fidia kwa Wafanyakazi, katika ofisi za WCF jijini Dodoma. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Hifadhi ya Jamii, Bw. Festo Fute.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Riziki Lulida akichangia jambo wakati wa majadiliano.

Mkurugenzi wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma akieleza jambo wakati wa Kikao cha kuwajengea uelewa wajumbe wa kamati hiyo kuhusu masuala ya Fidia kwa Wafanyakazi, katika ofisi za WCF, jijini Dodoma.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa na watendaji wa mfuko huo kuhusu masuala ya fidia kwa wafanyakazi.

Mnufaika wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. Godfrey Tamba (wa pili kushoto aliyesimama) akitoa ushuhuda wake mbele ya wajumbe wa Kamati katika Ofisi za WCF, jijini Dodoma.

About the author

mzalendoeditor