Featured Kitaifa

WAZIRI NDEJEMBI AAGIZA KUANZISHWA KITUO MAALUM KWA AJILI YA SHUGHULI ZA VIJANA

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Deogratius Ndejembi amewaagiza watendaji wa ofisi yake kuanzisha kituo maalum kwa ajili ya shughuli za vijana (START UP HUB) ikiwa ni mkakati wa kukuza na kuendeleza shughuli za maendeleo ya vijana nchini.

Mhe. Ndejembi ametoa agizo hilo leo Mei 17, 2024 Jijini Dodoma wakati wa kikao na Watendaji wa Ofisi yake pamoja na Taasisi ya Vijana ya Tanzania Startup Association kilicholenga kujadili mikakati ya kuendeleza shughuli za vijana.

Aidha, amebainisha kuwa kituo hicho kitasaidia kutatua changamoto wanazopata vijana katika biashara na shughuli zao za uzalishaji mali ikiwemo Kodi ya Pango na Leseni ya Biashara na hivyo kuhamasisha vijana waweze kushiriki katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo na itakayo wanufaisha kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuongeza fursa za ajira kwa vijana wenzao.

Katika Kikao hicho pia alishiriki Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana, Dkt. Mwiga Mbesi, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Bw. Amos Nyandwi pamoja na viongozi wa START UP wakiongozwa na Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo, Bw Zahor Muhaji.

About the author

mzalendoeditor