Featured Kitaifa

WAZIRI NAPE:WATUMIAJI WA HUDUMA ZA MAWASILIANO NCHINI WAMEONGEZEKA

Written by mzalendo
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye, akizungumza Bungeni jijini Dodoma, wakati akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2024/ 2025.
Na Mwandishi wetu, WHMTH 
Serikali imesema katika Mwaka wa Fedha 2023/2024 kumekuwa na mafanikio makubwa ya sekta ya habari na Mawasiliano, pamoja na upatikanaji wa mawasiliano nchini, hivyo kuongeza idadi ya laini za simu, watumiaji wa interneti na huduma za kutuma na kupokea fedha.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye, wakati akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya wizara kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 Bungeni jijini Dodoma tarehe 16 Mei, 2024.
“Sekta hii imeendelea kukua ambapo takwimu zinaonesha kuwa laini za simu zilizosajiliwa zimeongezeka kutoka milioni 62.3 Mwezi Aprili, 2023 hadi kufikia laini milioni 72.5 Mwezi Aprili, 2024, sawa na ongezeko la asilimia 16.4,” amesema Waziri Nape na kuongeza;
 “Mheshimiwa Spika kadhalika watumiaji wa intaneti wameongezeka kutoka milioni 33.1 Mwezi Aprili, 2023 hadi kufikia milioni 36.8 Mwezi Aprili, 2024 sawa na ongezeko la asilimia 11.2” .
Amebainisha kwamba katika kipindi hicho, pia watumiaji wa huduma za kutuma na kupokea pesa kwa njia ya mtandao wa simu wameongezeka kutoka milioni 44.3 hadi kufikia milioni 53.0 mwezi Aprili, 2024 sawa na ongezeko la asilimia 19.6..
Aidha, Waziri Nape amesema, idadi ya watoa huduma wa Miundombinu ya mawasiliano imefikia 25 ikilinganishwa na watoa huduma 23 waliokuwepo hadi Mwezi Aprili 2023, sawa na ongezeko la asilimia 8.7.
Amesema pamoja na mafanikio hayo, Serikali pia imefanikiwa kudhibiti mawasiliano ya simu ambapo simu za ulaghai 767 zimebainika na hatua stahiki zimechukuliwa kwa mujibu wa sheria.
Waziri Nape amesisitiza kuwa mafanikio hayo ya ongezeko la watumiaji wa huduma za mawasiliano yanayoonekana, yamechangiwa na juhudi mahsusi zinazofanywa na Serikali ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano katika maeneo yenye changamoto za kufikiwa.
Amesema, kwa mfano katika Mwaka wa Fedha 2023/24 Serikali ilianzisha ujenzi wa minara 758 katika kata 731 na kuongeza uwezo wa minara 304 kutoka teknolojia ya 2G kwenda 2G/3G na 4G.
Hadi Aprili 2024, minara 142 imekamilika kujengwa, kati ya hiyo, minara 124 tayari inatoa huduma na minara mingine 243 iliyokuwepo imeongezewa nguvu.
Amesema, Serikali pia imekamilisha upanuzi wa Mkongo wa Taifa kutoka ukubwa wa 200Gbps kwenda 800Gbps kwenye mizunguko mikuu ya Mkongo wa Taifa, na kuanza upanuzi wa Mkongo kutoka 800Gbps hadi 2000Gbps.

About the author

mzalendo