Featured Kitaifa

HALI YA SEKTA YA HABARI NCHINI IMEIMARIKA: WAZIRI NAPE

Written by mzalendo
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye, akizungumza Bungeni jijini Dodoma, wakati akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2024/ 2025.
Na Mwandishi wetu, WHMTH 
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amesema katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2023/2024, kumekuwa na ongezeko la vyombo vya habari lililochangiwa na Serikali kuendelea kuimarisha sekta ya hiyo nchini.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha Bajeti ya wizara kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025, Waziri Nape amesema vituo vya kurusha matangazo ya runinga vimeongezeka kutoka 65 mwaka 2023 na kufikia vituo 68 Aprili, 2024 sawa na ongezeko la asilimia 4.6.
Amesema, kwa upande wa Cable Television, zimeongezeka kutoka 57 Aprili 2023 na kufikia 60 Aprili 2024, sawa na ongezeko la asilimia 5.3. 
Kwa upande wa vituo vya kurusha matangazo ya radio, vimeongezeka kutoka vituo 215 mwaka 2023 hadi kufikia vituo 231 Aprili 2024 sawa na ongezeko la asilimia 7.4, na magazeti yameongezeka kutoka 321 Aprili 2023 na kufikia 351 Aprili 2024, sawa na ongezeko la asilimia 9.3. 
Aidha, Waziri Nape amsema, Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki ya matumizi ya teknolojia za utangazaji hasa maudhui mtandaoni yaliyochangia pia kuongeza ajira kwa vijana waliojikita katika sekta hiyo inayoendelea kukua kwa kasi. 
Kuhusu uhuru wa vyombo vya habari nchini, Waziri Nape amesema, umezidi kuimarika chini ya Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuhakikisha kuwa vyombo vya habari vinakuwa huru kupokea na kutoa habari za matukio mbalimbali yanayojitokeza katika jamii.
“Takwimu kutoka World Press Freedom lndex 2024 inayoratibiwa na Taasisi ya Reporters Without Boarders (RWB)(RSF) zimeonyesha kuwa Tanzania inaongoza kwa kuheshimu uhuru wa habari, Afrika Mashariki, na Kimataifa imeshika
nafasi ya 97 Mwaka 2024 toka nafasi ya 143 Mwaka 2023,” amesema Waziri Nape.
Amesema, kuheshimu uhuru wa vyombo vya Habari, kumechangiwa na Serikali kuchukua hatua muhimu ikiwemo kufanya mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya Mwaka 2016, iliyoridhiwa na Bunge mwaka 2023.

About the author

mzalendo