Akizungumza mara baada ya kutembelea katika Makao Makuu ya Tume ya kurekebisha ya Sheria na Tume Haki za Binadamu na Utawala Bora jijini Dodoma, Mei 8, 2024 Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini ameitaka Tume ya kurekebisha Sheria kujitangaza na kutoa elimu kwa wadau wa Sheria ili Tume iweze kushiriki ipasavyo katika kufanya mapitio ya Sheria mbalimbali.
Mhe. Sagini amesema kuwa ipo changamoto ya baadhi ya wadau wa Sheria kutokujua vizuri majukumu ya Tume na hivyo kuchelewa kuishirikisha Tume katika kufanya mapitio ya Sheria zao.
“Tume ipo kwa mujibu wa Sheria na Katiba yetu na inawajibu wa kufanya tathmini ya Sheria zilizopo kuona zile zilizopitwa na wakati, zinazohitaji marekebisho,utekelezaji wake na changamoto ili kuishauri Serikali namna bora ya kuboresha Sheria hizo.”Alisema Naibu Waziri Sagini.
Kuhusu utekelezaji wa miradi ya Maendeleo, Mhe. sagini amesema kuwa mpaka sasa Wizara kwa kushirikiana na Taasisi zilizopo chini yake zimeanza kuandika maandiko mbalimbali ili kuweza kuvutia fedha kutoka Serikali au wadau mbalimbali wa maendeleo na ameitaka Tume ya Kurekebisha Sheria kushiriki ipasavyo na kutoa mapendekezo yao katika miradi itakayopendekezwa.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Dr. Khatibu Kazungu amesema kwa kuwa Tafiti za Kisheria ni sehemu mojawapo ya majukumu ya Tume hivyo ni vyema wakaanzisha mashirikiano na Vyuo mbalimbali vya Elimu ya Juu vyenye kuhusu kada za Kisheria ili kufanya tafiti nyingi na kupata maarifa zaidi.