KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis.
NA MWANDISHI WETU,ZANZIBAR.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimempongeza kwa dhati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Mwinyi kwa kuendelea kujali na kuwajengea mazingira rafiki wafanyakazi nchini kwa kuanza kutoa posho ya nauli ya kuwapeleka kazini pamoja na kuongeza posho ya likizo.
Pongezi hizo zimetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo Zanzibar Khamis Mbeto Khamis, katika mahojiano maalum huko Afsini kwake Kisiwandui.
Alisema Chama Cha Mapinduzi kimeridhishwa na uamuzi huo wa busara,hekima,utu na mapenzi ya dhati kwa wafanyakazi nchini yatakayoongeza ari,ufanisi na uwajibikaji wenye viwango katika sehemu za kazi.
Katika maelezo yake Katibu huyo Mbeto, alisema Rais Dkt.Mwinyi ameendelea kuenzi kwa vitendo dhamira ya CCM ya kuhakikisha wananchi wa makundi mbalimbali wanaendelea kupata maendeleo endelevu bila ya kujali tofauti za kisiasa,kidini na kikabila.
“Tunampongeza sana Rais wetu Dkt.Hussein Ali Mwinyi kwa kazi kubwa anayofanya ya kuinua maslahi ya makundi mbalimbali hivyo nasaha zangu naomba tuendelee kumuamini na kumuunga mkono”, alisema Mbeto.
Alisema uongozi wa Dk.Mwinyi unaendelea kuandika historia kubwa na iliyotukuka nchini kwa kuchukuwa hatua, kuanza kutoa Posho la nauli za kwenda kazini na kurudi nyumbani ya TZS. 50,000 kwa watumishi wote wanaostahiki kulipwa posho na Jumla ya TZS. 34,099,500,000 zimetengwa na Serikali kwa ajili ya posho la usafiri.
Sambamba na hilo Rais wa Zanzibar Mwinyi ameeleza dhamira yake ya kuhakikisha serikali inaongeza fedha kwa ajili ya posho ya likizo ya jumla ya TZS. 2,523,814,700 zimetengwa na Serikali kwa ajili ya likizo katika bajeti mpya ya mwaka wa fedha 2024/2025.
Katibu huyo wa Idara ya Itikadi na Uenezi Zanzibar Mbeto, amesema kupitia hotuba ya Dk.Mwinyi,ameelezea hatua zilizopigwa na serikali katika kutimiza malengo ya kufikia ajira 300,000 zilizotajwa katika Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 ambapo kwa sasa tayari amefikia jumla ya ajira 187,651 sawa na asilimia 104 ya lengo la ajira 180,000 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Mbeto, alisema mafanikio yanayoendelea kupatikana katika sekta mbalimbali nchini yanatokana na matunda ya utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025.