Featured Kitaifa

THTU YATAKA HATUA KALI WANAOHUJUMU NHIF,YAIPA SERIKALI ANGALIZO KUHUSU KIKOKOTOO

Written by mzalendo
Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU), Dkt. Paul Loisulie,akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Uchambuzi na Mapendekezo ya hoja za NHIF na Pensheni nchini Tanzania.
Na Alex Sonna-DODOMA

KUELEKEA Bima ya Afya kwa Wote Chama  Cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu (THTU) imeshauri serikali kuendelea kuchukua hatua kali dhidi ya watu wanaotumia  vibaya fedha za mifuko ya bima ya afya ili kukomesha tabia hiyo.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa THTU Taifa Dk. Paul Loisulie, wakati akitoa  Mapendekezo ya Hoja Za NHIF na  Pensheni Nchini Tanzania.

Alisema pamoja na changamoto zote na dalili isiyo nzuri juu ya Bima ya Afya kwa  wote,  THTU inaamini kuna mambo ya kufanyika kwa utashi sahihi  na nia thabiti ili kuwezesha Bima ya Afya kwa wote ifanye kazi kwa  ufanisi mkubwa.

“Serikali iwe na hasira na wivu juu ya rasilimali zinazotapanywa  kila mara katika mifuko hii na kuchukua hatua ya kukomesha. 

Aliongeza kuwa :”Isisubiri ripoti ya CAG bali ichukue hatua mapema. Serikali pia  iepuke utaratibu wake wa kukopa au kujichotea pesa kutoka  kwenye mfuko ili pesa hizo zitumike kugharamia huduma za afya tun a si vinginevyo,”

Loisulie  alishauri   Bunge litimize wajibu wake kikamilifu katika kutunga sheria rafiki  kwa wafanyakazi na wanajamii Pamoja na kuisimamia serikali  katika usimamizi wa mifuko husika.

Alisisitiza kuwa Bunge halipaswi kuwa  sehemu ya kulalamika bali kutatua changamoto zinazojitokeza

Katika hatua nyingine alisema upo ulazima wa Wafanyakazi, wanajamii na wanufaika wote wa  Bima kuamka usingizini na kuacha tabia ya kugugumia chini kwa  chini huku Mfuko ukiteketea.

“Ijengeke tabia ya kuhoji na  kushinikiza uwajibikaji pale matumizi mabaya na usimamizi  usioridhisha inapobainika na mamlaka zinazoaminika kama CAG,”alifafanua . 

Aliongeza kuwa :” Ifanyike mijadala ya wazi na shirikishi kuhusu uhai wa mfuko  mara kwa mara ili kubaini changamoto na namna ya kuzitatua  badala ya kuachia mfuko peke yake. Hii itahusisha pia kutumia  ripoti za kitaalamu za tathmini juu ya mwenendo wa mfuko,”. 

Kuhusu Kikokotoo, (THTU) imependekeza Kikokotoo kifanyiwe mabadilko kwa kuongeza umri baada ya kustaafu toka miaka 12.5 hadi 15.5 na  wanachama wapewe angalau 50% kama mafao ya mkupuo.

 amesema “Kuhusu hoja ya Kikokotoo kinachotumika  hakiakisi hali halisi  ya wanachama – kanuni  8(1)(a)(b)(c) (a) kigezo cha umri (b) kigezo cha malipo  ya mkupuo mapendekezo yao ni Kikokotoo kifanyiwe mabadilko  kwa kuongeza umri baada ya kustaafu toka miaka 12.5 hadi 15.5.”amesema Dkt.Loisulie
Pia  wanachama wapewe angalau 50%  kama mafao ya mkupuo itumike 1/540 badala ya 1/580.
Kuhusu Waziri husika kuwa na  mamlaka ya kuamua kiwango cha michango ya mwanachama katika mfuko wanapendekeza Kifungu kidogo cha 18(2)(b) kiondolewe. 

About the author

mzalendo