Featured Kitaifa

SERIKALI KULIPA FIDIA ENEO LA IDEFU – MAKAMBAKO

Written by mzalendo

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alipokuwa akijibu swali bungeni jijini Dodoma.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – Wizara ya Fedha)

Na. Saidina Msangi, WF, Dodoma.

Serikali imesema kuwa imeanza taratibu za tathmini ya eneo la makaburi ya Idefu – Makambako na taratibu za malipo zitaanza baada ya kuidhinishwa na Mthamini Mkuu wa Serikali.

Hayo yameelezwa bungeni, jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Makambako Mhe. Deo Kasenyenda Sanga, aliyetaka kujua ni lini Serikali italipa fidia eneo la Makaburi Idefu – Makambako ili kupisha ujenzi wa One Stop Centre.

Mhe. Chande alisema kuwa Serikali tayari imeshalipa fidia ya shilingi bilioni 4.6 kwa wananchi waliopisha eneo kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa One Stop Centre.

Aidha, baada ya kupata majibu hayo Mhe. Sanga alitaka kujua kama Serikali itaona umuhimu wa kulipa fidia hiyo haraka kwa kuwa kiasi kilichobakia si kikubwa, huku akitaka kujua wakati ambao Serikali italipa madai ya fidia kwa wananchi Kilolo waliopisha ujenzi wa makao makuu ya wilaya ambayo yameshawasilishwa muda mrefu.

Mhe. Chande alisema kuwa tayari Serikali imeshalipa fidia kiasi cha Sh. bilioni 4.6 na kiasi kilicho baki ni Sh. milioni 100 na kumhakikishia Mhe. Mbunge huyo kuwa ndani ya mwaka huu wa fedha Serikali italipa fidia iliyobakia.

‘‘Kwa upande wa Kilolo Serikali iko tayari kulipa fidia hizo haraka inasubiri Mthamini Mkuu wa Serikali atoe idhini ili malipo yaweze kufanyika’’, alifafanua Mhe. Chande.

About the author

mzalendo