Featured Kitaifa

MASHAURI 705 YAOKOA TRILIONI 3.4 FEDHA ZA SERIKALI

Written by mzalendo

Na Mwandishi Wetu.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini ameipongeza Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali katika kusimamia na kushinda Mashauri 705 yenye madai ya fedha na kuipelekea Serikali kuokoa zaidi ya Shilingi Trilioni 3.47 kwa kipindi cha Julai 2023 hadi Aprili 2024.

Mhe. Sagini ameyasema hayo Aprili 19, 2024 wakati akifungua kikao cha pili cha Baraza pili la Wafanyakazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/ 2024 katika ukumbi wa mikutano wa NSSF, Mkoani Morogoro.

“Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imeonesha uzalendo na weledi katika kuhahikisha Serikali inashinda katika Mashauri na usuluhishi ndani na nje ya nchi.Fedha ambazo zimeokelewa ni mchango mkubwa katika kuisaidia Serikali kwenye utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.Niwapongeze kwa hatua hii na niwasihi tuendelee kulipigania Taifa.”Alisema Mhe. Sagini.

Aliendele kusema “Tunaishukuru sana Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi inavyoiwezesha Ofisi hii.Ongezeko la bajeti kutoka Shilingi Bilioni 17 zilizotengwa mwaka 2023/2024 hadi kufikia ukomo wa Shilingi Bilioni 20.7 kwa mwaka 2024/2025 takribani shilingi Bilioni 3.6 ni ishara kubwa kwamba Mhe. Rais anatambua mchango mkubwa wa Ofisi hii katika kuiwakilisha Serikali na Taasisi zake katika mashauri ya madai na usuluhishi”

Katika hatua nyingine Mhe Sagini amesema kupitia mikakati ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali katika kushughulikia mashauri ya ardhi Wizara ya Katiba na Sheria itaendelea kushirikiana na Wizara ya Ardhi ili kuendelea na jitihada za kupunguza migogoro ya ardhi kwa kuyashughulikia mapema kabla ya kuwasilishwa Mahakamani au katika mabaraza ya ardhi .

Kwa upande wake Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Luhende amesema kuwa Ofisi imeendelea kuwajengea uwezo Watumishi kwa kuwapatia mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi ikiwemo mafunzo ya kiubobevu katika maeneo maalumu ambapo kwa kipindi cha Julai 2023, hadi Aprili 2024 jumla ya Watumishi 11 wamepatiwa ufadhili wa mafunzo ya muda mrefu na watumishi 56 walipatiwa mafunzo ya muda mfupi ndani na nje ya nchi.

Aidha, Dkt. Luhende amesema upo uhitaji mkubwa wa Mawakili wenye ubobevu katika maeneo ya gesi,mafuta,uwekezaji,anga,madini,uchumi wa bluu,TEHAMA ili kuiwezesha Ofisi hiyo kufanya vizuri zaidi katika maeneo hayo ya kimkakati.

Awali akiwasilisha agenda kuu ya kikao hicho, Kaimu Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Ndg. Mark.Mulwambo amesema kuwa kikao hicho kinalenga kupitia na kujadili makadirio ya mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ambapo makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka huo ni Shilingi 20,750,720,000.Ofisi ikitaraji kutumia Shilingi Bilioni 4.3 na matumizi mengineyo yakitarajiwa kuwa Shilingi Bilioni 16.4.

Ikumbukwe kuwa, Mabaraza ya Wafanyakazi mahala pa kazi ni nyenzo muhimu katika kuboresha utendaji na ufanisi wa utekelezaji wa majukumu kwa Wafanyakazi.

About the author

mzalendo