Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Ally Gugu amekagua na kuridhishwa na ujenzi wa makazi ya Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, yaliyopo Kikombo jijini Dodoma ambapo, jumla ya majengo ya ghorofa sita yenye uwezo wa kuishi familia 60 yakiwa yamekamilika na majengo mawili yakiwa katika hatua ya msingi.
Akizungumza katika ukaguzi huo, Katibu Mkuu Gugu amesema kuwa ujenzi wa makazi hayo ya Askari ambao ni waajiriwa katika kada za awali za Jeshi lengo lake ni kuleta ustaarabu na staha kwa Askari hao na pia kuboresha na kuendelea kubadili taswira ya jiji la Dodoma kutokana na mwonekano wake.
“Nampongeza sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake.Thamani ya mradi huu kwa ukubwa wake unathamani ya fedha zisizopungua Shilingi bilioni 11. Mpaka sasa majengo sita yamekwisha kamilika ambapo jumla ya familia 60 zitakwenda kunuifa na makazi haya. Majengo mawili yatakayobeba familia 20 yapo katika hatua ya msingi na lengo la mradi ni kufikia familia 80. Hii ni motisha kwa Askari na inaonesha dhahiri jinsi Serikali inawajali Askari wake ikiwemo Askari wa Jeshi hili.”Alisema Gugu
Awali, akizungumza na Maafisa, Askari na Watumishi Raia katika kikao maalumu cha kujitambulisha na kufahamiana mara baada ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara, Gugu amewahimiza Watumishi kufanya kazi kwa ushirikiano kama timu moja, kuzingatia weledi na kuthamini jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuimarisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
Katika kutekeleza majukumu ya msingi ya Jeshi hilo, Gugu amesema Jeshi hilo halina budi kuendelea kushiriki ipasavyo katika udhibiti wa matukio ambayo yanaweza kuleta majanga na athari kwa binadamu na mali zake na hivyo amelielekeza Jeshi hilo kuendelea kujenga uelewa kwa kutoa elimu kwa jamii ili kuendelea kubaki salama.
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu Gugu ametembelea na kukagua ujenzi wa Jengo la Wizara Mtumba na kituo kipya cha Zimamoto na Uokoaji kilichopo Nzuguni, jijini Dodoma.