Featured Kitaifa

TEHAMA IWE KICHOCHEO KWENYE TATHMINI NA UFUATILIAJI WA TAKWIMU – DKT. JINGU

Written by mzalendoeditor

Na WAF, ARUSHA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu amesema Matumizi na Teknojia ya habari iwe ni kichocheo cha kufanya ufuatiliaji na tathmini ili kupata takwimu sahihi zitakazo changia kufanya maamuzi sahihi wakati wa kuandaa mipango ya bajeti kwenye Sekta ya Afya.

Dkt. Jingu amesema hayo wakati akifungua kikao cha siku mbili, Aprili 15, 2024 jiji Arusha, kilichowakutanisha wataalam wa Tehama na wale wa ufuatiliaji na tathmini zaidi ya 70 kwa lengo la kukuza ushirikiano baina ya wadau hao, uboreshaji wa program na maendeleo ya jumla ya utoaji wa huduma kwenye kwenye sekta ya afya ili kuwa na takwimu sahihi.

Dkt. Jingu amesema ukuaji wa Teknolojia uende sambamba na mabadiliko ya mifumo ya TEHAMA kwa kuiunganisha ili iweze kusomana hali itakayochangia kuwa na tija na ufanisi wakati wa utekelezaji wa majukumu kwenye sekta afya na kupata matokeo chanya.

“Chochote tunachofanya katika dunia ya leo lazima tutumie TEHAMA, kwetu sekta ya afya hii ni ajenda muhimu sana kutokana na unyeti wa shughuli zetu, kosa moja linaweza kusababisha kukosekana kwa huduma, ulemavu na wakati mwingine kupoteza uhai wa mtu, hivyo kikao kazi hiki kitumike kutoka na maazimio yatakayokuwa na tija na ufanisi”. Amesema Dkt. Jingu.

Dkt. Jingu amesisitiza juu ya mifumo ya Tehama kutengenezwa kulingana na mahitaji na kuzingatia teknolojia mpya na ya kisasa.

“Tusikimbilie kuanzisha mifumo mingi, tutumie mifumo iliyopo tuiboreshe ili iendane na wakati, mtakumbuka Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu, hivi karibuni alihimiza matumizi ya TEHAMA, sasa mnapokuwa na kikao hiki cha siku mbili mhakikishe mnachukua kama sehemu ya fursa ya majadiliano yenu muweze kutoka na maazimio.” Amesema Dkt. Jingu.

Akizungumza wakati wa kikao hicho Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) hapa nchini Dkt. Charles Moses amesema dunia imekuwa na mabadiliko mengi kwa muda mfupi, hivyo kila mabadiliko yanapotokea hususan ni kwenye Teknolojia ya habari na mawasiliano lazima vilevile na utendaji uendane na mabadiliko hayo.

“Tutumie fursa za Teknolojia kuhakikisha ajenda ya tahthmini na ufuatilaji inafanikiwa na hasa kwenye mipango yetu, Mlmipango ya Serikali inategemea sana ufuatiliaji na tathmini, nina imani tukiitanguliza Tehama katika hili tutafanikiwa”. Amesema Dkt. Charles.

About the author

mzalendoeditor