Na Gideon Gregory, Dodoma.
Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya usambazaji wa gesi asilia Jijini Dar es Salaam ambapo hadi sasa Serikali imeshasambaza gesi asilia kwa njia ya mabomba katika nyumba 880 katika Jiji la Dar es Salaam kwenye maeneo ya Sinza (226), Mikocheni (155), Kurasini (344) pamoja na Mwenge Mlalakuwa na Chuo Kikuu – UDSM (155).
Hayo yameelezwa leo Aprili 4,2924 Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Kawe Josephat Gwajima, aliyetaka kujua ni lini Serikali itaweka pipes za gesi Jijini Dar es Salaam kila nyumba ili wananchi wapikie nishati nafuu.
Aidha amesema Serikali imejenga bomba la gesi lenye urefu wa kilomita 12.4 kutoka Mwenge hadi Mbezi Beach kupitia barabara ya Bagamoyo ambapo Bomba hilo lina matoleo katika maeneo mbalimbali ili kuweza kuunganisha wateja wa majumbani.
“Kwa kuanzia tayari viwanda viwili (2) na hoteli sita (6) zimeshaunganishwa na bomba hilo katika eneo la Mbezi Beach na itaendelea kuunganisha wateja wa majumbani kwa maeneo yanayopitiwa na bomba hili,”amesema.
Amesema ili kuhakikisha wananchi wengi wanatumia gesi asilia, TPDC kwa kushirikiana na Kampuni ya TAQA Dalbit inafanya utafiti za mahitaji ya gesi asilia na njia za kusambazia katika Jiji zima la Dar es Salaam.
“Utafiti huo unatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2024 na utawezesha kuwa na mpango madhubuti wa usambazaji wa Gesi Asilia utakao zingatia changamoto ya mipango miji katika jiji la Dar es Salaam,”amesema.
Ameongeza kuwa Sekta Binafsi zinahamasishwa kushiriki kikamilifu katika uwekezaji ili kufanikisha ujenzi wa miundombinu na usambazaji wa gesi asilia katika maeneo mengi zaidi.