Featured Kitaifa

BILIONI 20.8 ZATENGWA KWAAJILI YA KULIPA POSHO ZA MADIWANI

Written by mzalendo

Na Gideon Gregory, Dodoma.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Afya Festo Ndugange amesema Serikali imetenga Jumla ya shilingi Bilioni 20.8 kwa ajili ya kulipa posho za Waheshimiwa Madiwani katika Halmashauri 168 ambapo kufikia Februari, 2024 kiasi cha shilingi Bilioni 13.5 kimetolewa.

Ndugange ameyasema hayo leo Machi 4,2024 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mhe. Flatei Gregory Mbunge wa Mbulu Vijiji ni lini Serikali itawalipa posho Wenyeviti wa Vitongoji na Vijiji na kuongeza posho ya Madiwani ili kuwasaidia kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Amesema Serikali inatambua kazi kubwa inayofanywa na Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji na Mitaa katika kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi.

“Serikali imeendelea kulipa posho za Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji na Mitaa ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ipasavyo, Katika mwaka wa fedha 2023/24, Serikali imetenga shilingi bilioni 1.7 ambapo kufikia Februari, 2024 shilingi bilioni 1.15 zimetolewa kwa ajili ya kulipa posho za Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji na Mitaa,”amesema.

Aidha, ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuongeza na kuboresha vyanzo vyake vya mapato ili kuendelea kulipa posho za Waheshimiwa Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji na Mitaa.

About the author

mzalendo