Featured Kitaifa

UDUMAVU NCHINI WAPUNGUA KUTOKA 34% 2018 HADI 30% 2022

Written by mzalendo

Na Gideon Gregory, Dodoma.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majiliwa amesema Serikali imeendelea kuimarisha mazingira wezeshi kwa wadau ili kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa afua za lishe, kwa kuzingatia malengo na shabaha za Mpango jumuishi wa Pili wa Taifa wa Lishe 2021/2022 – 2025/2026. 

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Aprili 3,2024 Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na Makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za ofisi ya Waziri Mkuu na ofisi ya bunge.

Majaliwa amesema Kupitia utekelezaji wa Mpango huo, utapiamlo kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano hususani udumavu umepungua kutoka asilimia 34 mwaka 2018 hadi asilimia 30 mwaka 2022, na utapiamlo mkali kufikia chini ya asilimia tano, sawa na malengo ya Shirika la Afya ya duniani. 

Amesema hadi kufikia Februari, 2024 Jumla ya shilingi bilioni 7.9 zilitolewa kwa ajili ya utekelezaji wa afua za watoto chini ya umri wa miaka mitano.

Aidha amesema kuwa kwasasa Tanzania imeanza kufanya Utafiti wa gharama ya Utapiamlo ikiwa ni utekelezaji wa maazimio ya viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kupitia mpango

ujulikanao kama “The Cost of Hunger in Study in Africa (COHA) ambapo Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi za mwanzo Barani Afrika kufanya utafiti huo muhimu.

“Utafiti huu unalenga kuinua dhana ya umuhimu wa kukabiliana na changamoto za utapiamlo miongoni mwa jamii barani Afrika kwa kubainisha gharama na athari zake kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi,”amesema. 

Amesema Matokeo ya utafiti huo pia yatatumika kama nyenzo bora ya uhamasishaji kwa viongozi wa Serikali na watunga sera kupitia

majukwaa mbalimbali ili kuchagiza hatua zaidi katika mapambano ya kutokomeza utapiamlo.

“Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutekeleza Mpango Jumuishi wa Pili wa Kitaifa wa

Masuala ya Lishe wa Mwaka 2021/22 – 2025/26, kufanya tafiti mbalimbali za kisayansi kuhusu masuala ya lishe, kuratibu vikao vya majadiliano

na mashirikiano na wadau wa lishe ili kufanya tathmini ya muda wa kati na kujadili utekelezaji Mpango huo pamoja na kupanga mikakati ya

pamoja itakayowesha Taifa kufikia malengo yaliyowekwa,”amesema.

About the author

mzalendo