Featured Kitaifa

WAZIRI NAPE AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA FINLAND TANZANIA

Written by mzalendo

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb.) akizungumza na mgeni wake Balozi wa Finland nchini Tanzania, Mhe. Theresa Zitting aliyeambatana na Mkuu wa Ushirikiano wa Ubalozi huo, Bw. Juhana Lehtinen na Mkurugenzi wa Nokia nchini Tanzania Amouneu Lopy kwa ajili ya mazungumzo yaliyofanyika leo katika Ukumbi wa Ofisi ndogo za wizara uliopo katika Jengo la TCRA jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb.) akipokea zawadi kutoka kwa Balozi wa Finland nchini Tanzania, Mhe. Theresa Zitting baada ya mazungumzo yaliyofanyika leo katika Ukumbi wa Ofisi ndogo ya Wizara uliopo katika Jengo la TCRA jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu , Dar es Salaam.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb.) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Finland nchini Tanzania Mhe. Theresa Zitting Ofisini kwake jijini Dar es Salaam aliyeambatana na Mkuu wa Ushirikiano wa Ubalozi huo, Bw. Juhana Lehtinen na Mkurugenzi wa Nokia nchini Tanzania Amouneu Lopy.

Mazungumzo hayo yamefanyika leo Machi 25, 2024 na yamehusisha ushirikiano baina ya Tanzania na Finland katika sekta ya TEHAMA hasa kwenye vipengele vya elimu ya TEHAMA, ubunifu na kukuza teknolojia na matumizi ya TEHAMA katika shughuli za kiuchumi na kijamii.

Waziri Nape amesema kuwa ushirikiano baina ya Finland na Tanzania umekuwa na mchango mkubwa katika kukuza Sekta ya TEHAMA nchini na kuzungumzia Mradi wa TANZICT (2011-2016) uliotekelezwa baina ya Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Finland ndio uliowezesha uandaaji wa Sera ya TEHAMA ya mwaka 2016.

Ameongeza kuwa sera hiyo ilikuwa msingi wa kutengeneza sheria nzuri zilizowezesha kukua kwa matumizi ya TEHAMA nchini. Hivyo, hatuwezi kuzungumzia mafanikio ya Sekta ya TEHAMA bila kuitaja Finland.

Viongozi hao walizungumzia pia masuala ya usalama mtandao, ulinzi wa taarifa binafsi, uchakataji wa taka za kielektroniki pamoja na kukuza matumizi ya vifaa janja vya kielektoniki kwa kuhakikisha vinapatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu ili matumizi ya TEHAMA yaende sambamba na uwekezaji unaofanyika.

About the author

mzalendo