Serikali ya Somalia imetangaza kwamba vikosi vya usalama vimewakamata washukiwa 16 kuhusiana na shambulio la kigaidi dhidi ya hoteli moja mashuhuri mjini Mogadishu.
Mashambulizi hayo yaliyoanza kwa milipuko ya mabomu na kufuatiwa na milio ya risasi siku ya Alhamisi, yalilenga hoteli ya SYL ambayo mara nyingi hutembelewa na maafisa wa serikali na wafanyabiashara walio karibu na ikulu ya rais.
Waziri wa habari Daud Aweis amesema katika taarifa yake kupitia mtandao wa kijamii wa X kwamba washukiwa waliokamatwa ni pamoja na Abdinasir Dahir Nur aliyepanga hujuma hiyo na wengine wanne.
Kundi la kigaidi lenye mafungamano na al-Qaeda, Al-Shabaab, lilidai kuhusika na shambulio hilo na kusema magaidi wake walivamia hoteli kwa mabomu na bunduki.
Magaidi hao walikaa ndani ya hoteli hiyo kwa karibu masaa 13 kabla ya kutimuliwa na vikosi vya usalama baada ya mapigano makali.
Wanajeshi watatu waliuawa katika shambulio hilo na watu 27 walijeruhiwa, wakiwemo wabunge watatu, kwa mujibu wa polisi.
Somalia imekuwa ikikabiliwa na ukosefu wa usalama kwa miaka mingi, huku vitisho vikuu vikitoka kwa al-Shabaab na makundi ya kigaidi ya Daesh au ISIS.
Magaidi wameongeza mashambulizi tangu Rais Hassan Sheikh Mohamud, ambaye alichaguliwa kwa muhula wa pili mwaka 2022, kutangaza “vita vya pande zote” dhidi ya kundi hilo.