Featured Kitaifa

WACHIMBAJI WA MADINI WA WATAKIWA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI

Written by mzalendo

Na Gideon Gregory, Dodoma.

Waziri wa Madini Anthony Mavunde amewahamasisha wachimbaji wa madini hasa yaliyokuwa na changamoto ya uchenjuaji na kulazimika kusafirishwa kwa mfumo wa makinikia, kuendelea kushirikiana kikamilifu na Serikali ili kuhakikisha lengo la ujenzi wa kiwanda cha usafishaji madini linatimia na linabaki kuwa alama ya ushindi katika usimamizi wa sekta ya madini.

Waziri Mavunde ameyasema hayo leo Machi 21,2024 Jijini Dodoma kwenye hafla ya kukabidhi leseni kubwa ya uchimbaji madini na leseni ya usafishaji madini ambapo ameongeza kuwa zoezi hilo linaenda kuongeza idadi ya leseni na kufikia 20.

“Ujenzi wa kiwanda cha multi metal refinery naamini itakuwa ni utatuzi wa changamoto iliyokuwepo kwa wachimbaji wa madini nchini kulazimika kusafirisha makinikia ya metali kwenda kwenye viwanda vya nje ya nchi kwa ajili ya uchakataji ili kupata zao la mwisho au kuuza madini katika hali ya makinikia kwa bei ya chini,”amesema Mavunde.

Aidha Waziri Mavunde ameongeza kuwa katika kuhakikisha kuwa changamoto zinazojitokeza kwenye sekta ya madini nchini Wizara inaendelea kufanya mazungumzo na wawekezaji wa nyanja mbalimbali ikiwemo utafutaji, uchimbaji na ujenzi wa viwanda vya usafishaji madini ili kuingia ubia na watanzania jambo litakaloongeza wigo wa upatikanaji wa mitaji, utaalam pamoja na uhaulishaji wa teknolojia.

“Nitumie nafasi hii pia kutoa wito kwa wachimbaji na wamiliki wa migodi inayozalisha makinikia nchini kutumia kiwanda hiki pindi kitakapo kamilika ili kukuza fursa za ajira na mapato yatokanayo na rasilimali madini, ameongeza Mavunde.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha amemuahidi Waziri wa Madini Anthony Mavunde kuwa atatoa ushirikiano kwa mamlaka zote katika kuhakikisha Fungani ya Buzwagi inakuwa na mafanikio makubwa kwa wananchi wa Wilaya ya Kahama.

RC Macha ameongeza kuwa wataendelea kuwahimiza wananchi wa Mkoa huo wa Shinyanga kuendelea kuchangamkia fursa zitakazojitokeza kupiti uwekezaji huo.

“Sambamba na uwekezaji mkubwa unaoenda kufanywa kule, na kama ambavyo tayari mmekwisha kunidokeza kuwa kampuni nyingi na kubwa zimekwisha onesha nia ya kuwekeza Mkoani Shinyanga sisi tunawihimiza wananchi wa pale wachangamkie fursa hii,”amesema.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Burian amesema kupitia uwekezaji huo uliofanywa na Serikali utaenda kuleta fursa mbalimbali kwa wananchi wa mkoa huo ikiwemo kujipatia ajira.

About the author

mzalendo