Featured Kitaifa

KAMATI YA LAAC YAITAKA HALMASHAURI YA MBULU KUTEKELEZA MAAGIZO ILIYOYATOA

Written by mzalendo

Na. Asila Twaha, Mbulu

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imeitaka Halmshauri ya Wilaya ya Mbulu kufanyia kazi ushauri na maagizo iliyoyatoa mara baada ya kamati hiyo kufanya ukaguzi na kubaini baadhi ya changamoto katika utekelezaji wa Mradi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu na Shule ya Sekondari Tumati.

LAAC imetoa maelekezo hayo Machi 17, 2024 wakati ilipofanya ziara ya kukagua miradi iliyotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya Mbulu Mkoani Manyara.

Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Ester Bulaya (Mb) amewahasa watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu kutekeleza kikamilifu majukumu yao pindi wanapopewa dhamana ya kusimamia fedha za umma katika utekelezaji wa mradi ili ikamilike kwa wakati na ubora pamoja na kuendana na thamani ya fedha iliyotolewa.

“ Hizi fedha za miradi ni za wananchi hivyo ni vema mkawa na uchungu nazo na kuzisimamia ili ziwe na tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi,” Mhe. Bulaya amesisitiza.

Awali, ikisomwa taarifa ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mbulu na ujenzi wa miundombinu ya Kidato cha Tano na cha Sita ya shule ya sekondari Tumati, Kamati iliitaka halmashauri hiyo kuondoa changamoto zote zilizobainiwa na kamati katika shule ya sekondari Tumati na kufuata taratibu na miongozo iliyotolewa na Ofisi ya Rais -TAMISEMI.

Aidha, kamati hiyo iliitaka halmashauri kukamilisha miundombinu ya maji kwenye vyoo katika shule hiyo ya Sekondari ya Tumati kabla ya kukamilika kwa mwaka huu wa fedha 2023/24.

Kwa upande wa utekelezaji wa mradi wa hospitali, Kamati imemuelekeza Mkurugenzi wa Halmshauri ya Wilaya ya Mbulu kuhakikisha fedha walizoingiziwa kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba zinatumika kama ilivyokusudiwa.

Kamati imeelekeza fedha shilingi milioni 500 zilizopokelewa kwa ajili ya ujenzi wa wodi tatu ambazo ni ya watoto, wanaume na wanawake zitumike kama ilivyopangwa na si kukamilisha miradi viporo.

Sanjari na hilo, LAAC imeitaka Ofisi ya Rais – TAMISEMI kushirikiana na Ofisi ya RAS kufanya tathmini ya kina kuhusu ufanisi wa utekelezaji wa miradi ili hatua stahiki iweze kuchuliwa dhidi ya wataalamu waliohusika kukwamisha utekelezaji wa miradi.

Naye, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais -TAMISEMI Dkt. Charles Msonde ameihakikishia Kamati ya LAAC kuwa, TAMISEMI itafuatilia na kusimamia utekelezaji wa maelekezo ya kamati ili thamani ya fedha ionekane na wananchi wanufaike na miradi.

About the author

mzalendo