Kitaifa

AHUKUMIWA MIAKA 30 JELA KWA KOSA LA KUBAKA

Written by mzalendo

Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi imemhukumu mshtakiwa Swetbert Kasanga (29) Mkazi wa mtaa wa Tulieni Halmashauri Wilaya ya Mpanda kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka kibibi kizee wa miaka 89.

Hukumu hiyo imetolewa Machi 14, 2024 na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo Mhe. Gasper Luhoga.

Akisoma hukumu hiyo Mhe. Luhoga alisema mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Disemba 26, 2023 huko katika mtaa wa Tulieni kwa kumvizia kizee huyo akiwa ndani kwake kisha kuvunja mlango kuingia ndani na kumfanyia unyama huo.

Mshtakiwa huyo mara baada ya kutenda tukio hilo alikimbia kusikojulikana ambapo Jeshi la Polisi likifanya juhudi za kumtafuta na Disemba 27, 2023 alikamatwa.

Mhe. Luhoga amesema Mshtakiwa huyo ametenda kosa hilo chini ya kifungu namba 130 sura ya 16 cha sheria ya kanuni ya adhabu kilichofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Kesi hiyo ilikuwa na jumla ya mashahidi watano ambapo Mhe. Luhoga alisema mahakama imefikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha na ushahidi uliotolewa pasipo shaka.

Kesi hiyo ilifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Januari 11, 2024 na kusajiwa kwa kupewa namba kesi ya jinai 853 mwaka 2024.

About the author

mzalendo