Featured Kitaifa

UGONJWA WA FIGO WASHIKA NAFASI YA NANE DUNIANI KUSABABISHA VIFO

Written by mzalendo

Inakadiriwa kuwa watu milioni 850 duniani wanasumbuliwa na magonjwa sugu ya figo na kati yao watu milioni 3.1 hufariki dunia kila mwaka na kuufanya ugonjwa huo kushika nafasi ya nane ulimwenguni kwa kusababisha vifo.

Hayo yamesemwa leo na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo kutoka Hospitali ya Muhimbili, Dkt. Jonathan Mngumi wakati akitoa elimu kuhusu umuhimu wa kulinda na kutunza figo dhidi ya magonjwa ikiwa ni siku ya maadhimisho ya figo Duniani ambayo huadhimishwa mwezi machi kila mwaka.

Ameeleza kuwa watu wengi wenye magonjwa ya figo wanakadiriwa kuishi katika nchi zinazoendelea hususani kusini mwa Jangwa la Sahara na idadi hiyo imekuwa ikiongezeka kila mwaka na kwa sasa inakadiriwa kuwa wastani wa asilimia 7 mpaka 25 ya wakazi wa Afrika wana matatizo ya figo ambapo kiasi hiki ni mara tatu zaidi ya nchi zilizoendelea, amesema Dkt. Mngumi

“Idadi ya wagonjwa wanaopatiwa huduma ya kusafisha damu imefikia 3,500 nchini kote ambapo kwa Muhimbili kila siku inahudumia wagonjwa 120 hadi 130,” amesema Dkt. Mngumi.

Dkt. Mngumi ameitaka jamii kubadili mtindo wa maisha kuacha matumizi makubwa ya sigara, unywaji wa pombe kupita kiasi na kufanya mazoezi mara kwa mara ili kujikinga na magonjwa mbalimbali kama vile kisukari na shinikizo la damu ambayo yameonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa magonjwa ya figo.

Kauli mbiu mwaka ya huu inasema “Afya ya figo kwa wote, kuendeleza usawa katika ufikiaji wa huduma na matumizi bora ya dawa”

 

About the author

mzalendo