Featured Kitaifa

TAASISI ZATAKIWA KUWA NA USHIRIKIANO NA HALMASHAURI

Written by mzalendo

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imetoa wito kwa taasisi kuwa na ushirikiano wa uratibu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye halmashauri zao.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati, Mhe Denis Londo wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kukagua utekelezaji wa miradi ya elimu, afya na miundombinu katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi na Halmashauri ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro leo.

Mhe Londo amesema ni vema halmashauri inapokua inatekeleza miradi ya elimu ama afya kuwasiliana na wenzao wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA, TANESCO na taasisi zingine ili nazo zianze mchakato wa kupeleka huduma ili kuleta manufaa na tija kwa wananchi.

“ Nizipongeze Halmashauri zote mbili kwa utekelezaji wa miradi hii, TARURA Mkoa mmefanya kazi kubwa sana hongereni. Lakini ni vema kukawa na uratibu wa pamoja kwa taasisi za Serikali. Haiwezekani hapa hospitali inajengwa halafu TARURA hamrekebishi barabara, au Shule inajengwa inakamilila lakini watu wa idara ya maji wanakua hawajaleta huduma. Tunaomba huduma zote ziende pamoja,” Amesema Mhe Londo.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Deogratius Ndejembi ameishukuru kamati hiyo kwa kutembelea na kukagua miradi hiyo sambamba na kutoa ushauri huku akiahidi kuwa watasimamia kwa weledi maelekezo yote yaliyotolewa na kamati.

Ziara hiyo imehudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI anayeshughulikia miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila ambapo miradi iliyotembelewa ni pamoja na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Moshi, Shule ya Sekondari Saashisha iliyopo wilayani Hai na ujenzi wa barabara ya Makoye-Mferejini.

About the author

mzalendo