Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, uwekezaji wowote unaofanywa katika Sekta ya Elimu lazima umguse Mwalimu kwani ndiye injini na kiongozi wa rasilimali zote zinazowekwa kwenye mfumo wa elimu nchini.
Dkt. Biteko mesema hayo tarehe 13 Machi 2024 wakati alipomwakilisha Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika hafla ya kuzindua Programu ya Kuboresha Kada ya Ualimu nchini (GPETSP) katika Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam hafla ambayo ilienda pamoja na kaulimbiu ya Walimu Wetu Fahari yetu.
“Mwalimu ndiye rasilimali kuu inayofanya rasilimali nyingine ziweze kuleta matokeo chanya kwenye Sekta ya Elimu, ndio maana mtaona programu tunayoizindua leo inaonesha kwa vitendo kuwa Serikali tunatambua kwamba lazima tuwekeze zaidi kwa Walimu kwenye mazingira ya kujifunza na ufundishaji lakini pia kuwatambua Walimu kuwa ninyi ndio watu tunaowategemea kufanya elimu yetu iweze kwenda mbele.” Amesema Dkt. Biteko
Amesema, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya kila jitihada ili masuala yote yanayowahusu Walimu yafanyiwe kazi kwa kasi ikiwemo kuwapunguzia changamoto zinawazowakabili ili Walimu hao wajikite katika kusomesha na kutatua changamoto za watoto mashuleni.
Ameongeza kuwa, kutokana na kazi nzuri ya Walimu hapa nchini, ufaulu wa wanafunzi kutoka Shule ya Msingi kwenda Sekondari umeongezeka kutoka 907,802 mwaka 2021 hadi 1,092,984 mwaka 2023 ikiwa ni ongezeko la asilimia 20.4.
Dkt. Biteko ameeleza kuwa, Serikali inaendelea kuboresha bajeti ya Elimu ambapo katika mwaka 2021 fedha iliyotolewa ni shilingi Trilioni 4.7 na kwa mwaka 2023 imeongezeka hadi shilingi Trilioni 5.7 sawa na asilimia 20.4.
Kuhusu ajira kwa Walimu amesema kuwa, zimeongezeka ambapo katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita Walimu 37,473 wa Sekondari na Msingi wameajiriwa, Walimu 227,383 wamepandishwa madaraja na Walimu 20 wamebadilishiwa vyeo.
Amesema pamoja mafanikio hayo bado kuna changamoto kwenye Sekta ya Elimu ikiwemo ya kuongezeka kwa udahili wa wanafunzi ambao unahitaji ongezeko la Walimu na miundombinu mingine ikiwemo madarasa na nyumba za Walimu na kueleza kuwa Serikali inatambua bado kuna kazi kubwa ya kufanya katika Sekta ya Elimu ambapo ametoa wito kwa wadau kushirikiana na Serikali ili kuimarisha mahitaji ya Elimu nchini.
Dkt. Biteko amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inawajali Walimu nchini na ndio maana inatekeleza vipaumbele Nane ili kuboresha kada hiyo ikiwemo ujenzi wa nyumba za Walimu kwenye Halmashauri za pembezoni, kuimarisha mfumo wa motisha kwa walimu ili kuwafanya wabaki kwenye kazi yao, kuwezesha uandaaji wa mfumo jumuishi wa kieletroniki wa uandaaji, usimamizi na upangaji wa Walimu kwa kuzingatia usawa wa kijinsia na kuwezesha utekelezaji wa mpango wa ajira kwa walimu wa kujitolea kwa ajili ya kupungiza changamoto za upatikanaji wa walimu msingi ili kuimarisha mazingira ya kujifunza na ufundishaji.
Ametaja vipaumbele vingine kuwa, ni kumwezesha Mwalimu kufanya upimaji wa kielektroniki ili kupata matokeo ya kila hatua ya kujifunza, kujenga vituo vya walimu na kuweka samani na vifaa vya kielektroniki ili kuwezesha mafunzo endelevu kwa walimu waliokazini, ununuzi wa zana na vifaa visaidizi kwa Wakufunzi, Walimu, Walimu tarajali na wanaofundisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu pamoja na kutoa ufadhili wa masomo kwa walimu wanaofundisha wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Dkt. Biteko amempongeza Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia Masuala ya Elimu Duniani (GPE), Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na kueleza kuwa nafasi aliyonayo ni heshima kwa nchi pamoja na Sekta ya Elimu nchini kwani amekuwa na mchango katika kuhakikisha nchi inafaidika na mfumo wa GPE ambao unahudumia nchi 89 duniani.
Katika hatua nyingine, Dkt. Doto Biteko ameziagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na TAMISEMi kuangalia utaratibu mzuri wa kuwapa motisha Walimu na hii ikihusisha kutenga walau siku moja ya kuwapa Motisha walimu hao badala kusubiri Mei Mosi kwa lengo la kupata matokeo yaliyo bora kwenye Sekta ya Elimu.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia Masuala ya Elimu Duniani (GPE), Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema kuwa, lengo la Taasisi hiyo ni kusaidia kuchochea maendeleo ya elimu katika nchi zinazoendelea hasa za kipato cha chini na za kipato cha kati hatua ya kwanza ambapo Tanzania ni moja ya nchi 89 wanufaika wa GPE.
Amesema kuwa, kutoka GPE ianze mwaka 2002 imeshachangia Dola za Marekani milioni 330 nchini Tanzania na kwamba GPE inaunga mkono juhudi za Serikali kuboresha Sekta ya Elimu ili kila mtoto nchini awe na ujuzi na maarifa na sasa Taasisi hiyo imeidhinisha ufadhili wa Dola za Marekani Milioni 80 kwa ajili ya programu ya GPETSP.
Awali, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alisema kuwa, programu iliyozinduliwa ya GPETSP inagusa sehemu mbalimbali katika Kada ya Ualimu ikiwemo kuhakikisha kunakuwa na utoshelevu wa Walimu, ubora, uwepo wa miundombinu, vitendea kazi, kuendeleza makazi ya walimu na motisha kwa walimu na kwamba Serikali imekuwa ikiyafanyia masuala hayo lakini GPETSP inakuja kuongeza nguvu na kasi ya utekelezaji wa programu za Serikali ikiwemo Sera ya Elimu.