Featured Kitaifa

UNICEF YAAHIDI KUSAIDIA UTEKELEZAJI MAGEUZI KATIKA SEKTA YA ELIMU

Written by mzalendo

Shirika la Kimataifa la Kuhudunia Watoto (UNICEF) limeahidi kusaidia utekelezaji wa mageuzi katika sekta ya elimu ili kuhakikisha watoto wa kitanzania wanapata elimu bora.

Hayo yameelezwa Machi 12, 2024 Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini wa Shirika hilo Etleva Kadili alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ambapo amesema wanatambua juhudi kubwa imefanyika na hivyo ni lazima ziungwe mkono ili kufikia malengo.

Kadili ameongeza kuwa serikali ya Tanzania imepiga hatua kubwa katika katika kuhakikisha watoto wote wanapata elimu bila vikwazo vyovyote na kupongeza hatua ya kuwarudisha shule wanafunzi waliokatisha masomo yao kutokana na changamoto mbalimbali

“Tumekuja hapa kuwapongeza kwa jitihada kubwa mlioifanya ya kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya elimu nataka, nikuhakikishie kuwa UNICEF ipo tayari katika kusaidia utekelezaji wa mageuzi haya” amesisitiza Kadili.

Aidha, Mkurugenzi huyo amesema UNICEF itaendelea kusaidia katika mafunzo ya walimu na kutekeleza afua zitazowezesha kupunguza mdondoko wa wanafunzi katika shule.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amemweleza Mkurugenzi huyo kuwa Serikali imeanza utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 pamoja na Mitaala mipya kwa Elimu ya Awali, Darasa la kwanza , la tatu na Sekondari Mkondo wa Amali.

Prof. Mkenda ameongeza kuwa kwa sasa Serikali inafanya utafiti kuangalia juu ya mdondoko wa wanafunzi ili kuweza kubaini sababu na kuzipatia utatuzi ili kuondoa changamoto hiyo.

About the author

mzalendo