Kitaifa

RAIS DKT. SAMIA KUBEBA AJENDA YA MATUMIZI YA NISHATI SAFI

Written by mzalendo

Na. Gideon Gregory, Dodoma.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa TanzaniaDK Samia Suluhu Hassan ameahidi kuibeba ajenda ya Afrika ya matumizi ya Nishati safi ili kuitunza misitu na kuhifadhi mazingira hivyo ataendelea kutafuta fedha kwaajili ya kukuza matumizi ya nishati safi yakupikia.

Dk.Samia ametoa kauli hiyo leo Machi 9,2024 kwa njia ya simu wakati akizungunza na Makamu wa Rais Dk.Philip Mpango Jijini Dodoma katika Kongamano la wanawake la kugawa mitaji na vitendea kazi vya nishati safi ya kupikia.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema mwathirika mkubwa wa athari zitokanazo na matumizi ya nishati chafu ya kupikia ni mwanamke hivyo kuna haja ya kupunguza gharama ya gesi.

“Katika maeneo mengi ya vijijini, kina mama hutumia muda mwingi kutafuta kuni na hivyo kushindwa kujihusisha na shughuli za maendeleo. Pia, utafutaji huo huhatarisha maisha yao pale wanapokumbana na wanyama wakali wa porini pamoja na ukatili wa kijinsia”, amesema.

Aidha vilevile ameongeza kuwa mama huyo huyo ambae huvuta moshi wenye viwango vikubwa vya sumu wakati wa kupika, akiwa na mtoto mdogo jikoni, mtoto naye anaweza kudhurika vile vile.

Ameongeza kuwa athari hizo huchangia magonjwa yanayopelekea vifo takribani 33,000 vya watanzania kila mwaka, ambapo asilimia kubwa ya vifo hivyo ni kina mama na watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambao hutumia muda mwingi jikoni na mama zao wakati wa kupika.

“Hivyo, athari hizi huchangia magonjwa yanayopelekea vifo takribani 33,000 vya watanzania kila mwaka, ambapo asilimia kubwa ya vifo hivi ni kina mama na watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambao hutumia muda mwingi jikoni na mama zao wakati wa kupika,”amesema.

Naye Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Waziri wa Nishati Dtk. Doto Biteko ameeleza umuhimu wa matumizi ya Gesi asilia huku akitoa maagizo kwa wakuu wa mikoa na wilaya kubeba ajenda ya nishati mbadala kama chanzo cha utunzaji wa mazingira.

“Hebu tuibebe hii ajenda kwa pamoja Wakuu wa Mikoa, Viongozi wa dini katika mahubiri yenu tafuteni sentensi mbili tatu kuwaambia waumini wenu umuhimu wa matumizi ya Nishati safi,wakina Baba nyumbani wakati mnazungumza na watoto wapeni sentensi mbili tatu wakue wakijua umuhimu wa matumizi ya Nishati safi”.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Ndg. Mary Chatanda (MCC) ameiomba Serikali kupunguza bei ya Nishati ya gesi ili wanawake Waweze kuachana na Matumizi ya kuni na mkaa kwenye shughuli za mapishi.

Amesema Bei ya Nishati safi ya Gesi ya kupikia ikipungua tofauti na ilivyo kwa sasa basi wananchi wengi wakiwemo wanawake wataweza kununua majiko na kuachana na Matumizi hatarishi ya kuni.

“Bei ya gesi ikipunguzwa madukani wanawake watakuwa na uwezo wa kununua kila yanapoisha na yatakuwa yanatumika nasio kuwa mapambo majumbani kwetu kama ilivyo sasa.”

 

About the author

mzalendo