Featured Kitaifa

ZUCHU AFUNGIWA KAZI ZA SANAA ZANZIBAR

Written by mzalendo

 

Katibu mtendaji baraza la sanaa sensa ya filamu na utamadini Dkt. Omar  Abdalla Adam akitoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya hatua za kumfungia msanii Zuhura Othman Soud (ZUCHU) kufanya kazi za sanaa Zanzibar kufuatia kukiuka mila,silka na utamaduni wa kizanzibari, huko Ofisi za BASFU  Mwanakwerekwe.

Mrajis Baraza la sanaa sensa ya filamu na utamadini Juma chum juma akifafanua  hatua za kufungiwa  msanii Zuhura Othman Soud (ZUCHU) kufanya kazi za sanaa Zanzibar katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ofisi za BASFU  Mwanakwerekwe.

PICHA NA FAUZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR 

Na Rahma Khamis Maelezo Zanzibar 

Baraza la Sanaa, Sensa ya Filamu na Utamaduni Zanzibar limemfungia Msanii wa Bongo Fleva Zuhura Othman Suod (ZUCHU) kwa muda wa miezi sita na kulipa faini ya shiling  milioni moja za kitanzania  kutokana na kuimba nyimbo zisizokuwa na maadili na maudhui mazuri kwa vijana wa kizanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari huko Ofisini  kwake Mwanakwerekwe Wilaya ya Magharib B’ Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Dkt Omar Abdalla Adam amesema hatua hiyo imekuja baada ya kufanya onyesho la burdani  katika Kijiji cha Kendwa huko Hoteli ya Kendwa Fullmoon Part na kuonesha ishara zisizo na maadili na kuvaa vazi la uchi kitendo ambacho sio kizuri pamoja na kuimba nyimbo zisizo na maadili jambo ambalo ni kosa kisheria.

Amesema kwa mujibu wa kifungu namba  8 (1),(d) cha sheria nambari 7 ya 2015 ya Baraza la Sanaa, Sensa ya Filamu na Utamaduni Zanzibar, lina haki ya kumfungia msanii huyo kutokana na kukiuka sheria zilizowekwa za kuimba nyimbo zinazozingatia mila silka na Utamaduni wa Mzanzibari.

 Katibu huyo amefahamisha kuwa msanii huyo hana usajili  kwa hapa Zanzibar katika utendaji  wa kazi zake na wala hana mashirikiano ya aina yeyote katika Baraza hilo hivyo Baraza la Sanaa, Sensa ya Filamu na Utamaduni Zanzibar limemfungia Msanii huyo na kumtaka kufika Zanzibar  kuomba radhi na endapo atakwenda kinyume na agizo hilo hatua kali  zitachukuliwa dhidi yake.

Aidha Katibu ameitaka jamii ya Kizanzibar kupuuuza na kutosikiza nyimbo za msanii huyo  pamoja na kundi lake kwani kuendelea kuzisikiliza na kuimba nyimbo hizo ni kuharibu mila na utamaduni uliopo.

Nae Mrajisi wa Baraza hilo Juma Chuom Juma amesema  kwa mujibu wa Ibara namba 8 (B) inalitaka Baraza kuchukua hatua  kwa  wasanii wanaokuja  kuimba Zanzibar bila ya kufuata utaratibu uliyopo  kwani kuna sheria na utamaduni wake hasa ukizingatia kwamba  kipindi kinachokuja cha mwezi mtukufu wa Ramadhan.

About the author

mzalendo