Kimataifa

Written by mzalendo

Watu 13 walifariki siku ya Ijumaa usiku baada ya mtumbwi wao kuzama kwenye Mto Kongo karibu na eneo la mto Lubunga huko Kisangani (Tshopo). Wengi wa waathiriwa ni wanawake na watoto. Abiria wengine kadhaa hawajulikani waliko, kulingana na radio OKAPI ikinukuu vyanzo vya ndani huko Lubunga.

Mtumbwi uliopinduka ulikuwa ukitokea katika mji wa Isangi-Makutano, ulioko karibu ya mto Kongo.

Sababu za ajali hii bado hazijafahamika.

Kulingana na Crown Prince Isomela, kiongozi wa shirika lisilo la kiserikali la Sauti ya Lubunga, mtumbwi huo uligongana na mtumbwi mwingine uliokuwa ukielekea upande wa chini kutoka eneo la Wagenya.

Hata hivyo, shahidi mmoja aliyenukuliwa na radio Okapi, ameripoti kuwa mawimbi kutoka Wagenya Falls ndiyo chanzo kikuu cha ajali hiyo.

Idara ya usalama ya Lubunga inabainisha kuwa mtumbwi huu ulikuwa umebeba zaidi ya watu 30 na mizigo.

Baadhi ya miili ilipatikana Ijumaa hiyo hiyo jioni. Miili mingine imeokolewa leo Jumamosi asubuhi na waogeleaji.

Watu saba waliokolewa huku wengine kadhaa wakikosekana, mmiliki wa mtumbwi huu hakuweza kupatikana hadi Jumamosi hii asubuhi, Machi 2. Idara za serikali zilikuwa zikimtafuta.

Shirika lisilo la kiserikali la Sauti ya Lubunga linasikitika kwamba baadhi ya wamiliki wa boti zinazofanya shughuli la kuvusha watu na bidhaa kwenye kingo zote mbili za Mto Kongo hawaheshimu maagizo katika suala hili. Hasa kuhusu idadi ya watu wanaopaswa kusafirishwa pamoja na saa za shughuli hiyo.

About the author

mzalendo