Kimataifa

31 WAPOTEZA MAISHA KATIKA AJALI YA BARABARANI NCHINI MALI

Written by mzalendo

Watu wasiopungua 31 wamepoteza maisha katika ajali mbaya ya barabarani iliyotokea magharibi mwa Mali.

Kwa mujibu wa Wizara ya Uchukuzi ya Mali, basi la uchukuzi wa umma lilkilokuwa likielekea katika nchi jirani ya Burkina Faso lilipoteza muelekeo na kutumbukia kwenye Mto Bagoe katika mji wa magharibi wa Kenieba.

Taarifa ya wizara hiyo imeeleza kuwa, raia wa Mali na nchi nyingine za Afrika Magharibi ni miongoni mwa watu walioaga dunia kwenye ajali hiyo iliyotokea mwendo wa saa 11 jioni hapo jana.

Takwimu zinaonyesha kuwa, kila mwaka mamia ya watu hufariki dunia katika ajali za namna hiyo nchini Mali, suala lililoifanya polisi ya nchi hiyo kuweka sheria kali za barabarani kukiwemo kuwatoza faini kubwa madereva wanaokiuka sheria za trafiki. 

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), watu 3,200 wanaaga dunia kila siku katika ajali za barabarani katika pembe mbalimbali za dunia.

Kiwango hicho kikubwa cha maafa ya barabarani kimeibua mijadala ya wazi juu ya wajibu wa kuimarishwa miundombinu, utekelezaji mkali wa sheria za barabarani, elimu ya kina kwa madereva, na uwekaji wa viwango vikali vya usalama wa magari kabla hayajaingia barabarani.

About the author

mzalendo