Featured Kitaifa

WASAJILI WA BODI NA MABARAZA YA TAALUMA WATAKIWA KUSIMAMIA UTENDAJI NA MAADILI

Written by mzalendo



Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. John Jingu amewataka Wasajili wa Mabaraza ya Wataalamu na Bodi ya Washauri nchini kuweka mikakati na mfumo wa kuhakikisha unawafikia na kufuatilia utendaji kazi wa wataalam katika sekta ya Afya na kuwachukulia hatua watakao bainika wanakwenda kinyume na maadili ya utendaji wa kazi zao ili kulinda sekta na kuhakikisha watanzania wanapata huduma za afya zilizo bora.

Dkt. Jingu amesema hayo Februari 22, 2024 jijini Dodoma katika kikao na Wasajili wa Mabaraza ya wataalam na Bodi ya Washauri kilichokua na lengo la kujadili namna ya kuzidi kuboresha huduma kwa wananchi.

Amesema kuna kesi nyingi zinatokea katika maeneo ya kazi ambapo kuna wanataaluma, wasajili na wasimamizi wa bodi na mabaraza wanatakiwa kuwatembelea ili kujua changamoto zinazowakabili wasisubiri kesi zifike kwenye Mabaraza yao wakiwa ofisini.

“Nendeni mkatembelee wataalamu katika maeneo yao ya kazi mkaone wanavyofanya kazi, msijifungie maofisini na msiwe mahakimu wa kusubiri hadi matatizo yatokee ndio mchukue hatua”. Amesema Dkt. Jingu.

Ameongeza kuwa mtaalam atakaegundulika hafuati maadili achukuliwe hatua mara moja ili asiharibu taaluma na.kusababisha wananchi kupata huduma bora.

Dkt. Jingu ameelekeza mabaraza kujitangaza ili kujulikana majukumu yake na kuwawekea namna nzuri wananchi waweze kuwafikia na kuongeza ufanisi wenye tija katika kushughulikia kero za wananchi.

“Twendeni tukawajulishe wananchi juu ya sisi ni wakina nani, majukumu yetu ni yapi na njia na mawasiliano wanayoweza kutumia ili kutufikia, pia msicheleweshe mashauri ambayo yanaletwa kwenye mabaraza yenu. Ongezeni ufanisi katika kutatua changamoto za wananchi kwa muda mfupi”. Amesema Dkt. Jingu.

Mwisho. Dkt. Jingu ameongeza kuwa kuna Baadhi ya watumishi wa Sekta ya afya wamekuwa wakikiuka Maadili ya kiutumishi na kuleta mkanganyiko kwa jamii hilo ni moja ya jukumu la Mabaraza kuhakikisha weledi unakuwepo kwa wataalam mnaowasajili.

Awali akimkaribisha Katibu Mkuu kwenye kikao hicho, Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu amesema ofisi ya Mganga Mkuu wa Serikali chini ya Wizara ya Afya ina jukumu la kusimamia Mabaraza nane ya kitaaluma ambapo miongoni mwa jukumu ni kusimamia weledi na maadili ya wataalamu pamoja na Bodi mbili za Washauri ambazo ni Bodi ya Maabara Binafsi (PHLB) na Bodi ya Ushauri wa Hospitali Binafsi (PHAB) zenye jukumu la kumshauri Waziri juu ubora  wa huduma na kusajili maabara na hospitali binafsi.

About the author

mzalendo