Wagombea 15 kwenye uchaguzi ulioahirishwa nchini Senegal wamemshtumu Rais Macky Sall kuwa na nia mbaya na wameapa kuchukua hatua kuhakikisha tarehe mpya ya uchaguzi inatangazwa kwa haraka.
Tangazo hilo limetolewa huku muungano wa mashirika ya kiraia ulioanzisha kampeni iitwayo Tulinde uchaguzi wetu ukisema kwamba umepanga maandamano mapya Jumamosi wiki hii.
Muungano huo unaomba uchaguzi ufanyike kabla ya muhula wa Macky Sall kumalizika hapo Aprili 2.
Unasema uchaguzi ambao awali ulipangwa kufanyika Februari 25 lazima ufanyike ifikapo tarehe 3 mwezi Machi.
“Kumeonekana nia isiyoeleweka ya kutaka kuchelewesha mambo. Hakuna kilichofanyika licha ya hatua iliyopigwa wiki iliyopita, wagombea hao 15 walisema katika taarifa ya pamoja Jumanne jioni.
“Kila kitu kinakwenda kwa kasi ya nia mbaya ya Rais Macky Sall,” taarifa hiyo iliongeza.
Wagombea hao 15 waliosaini taarifa hiyo ni pamoja na Meya wa zamani wa mji wa Dakar Khalifa Sall na mgombea wa upinzani anayezuiliwa jela Bassirou Diomaye Faye, ambaye jina lake liliongezwa na mshirika wake wa karibu.
Faye ni naibu wa kiongozi wa upinzani Ousmane Sonko, ambaye yuko gerezani pia.