Takwimu zilizowasilishwa katika Bunge la Kenya zimeweka wazi kuwa Tume ya Huduma za Walimu (TSC) imelipa Shilingi milioni 466 kama mishahara kwa walimu-hewa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.
Stakabadhi zilizowasilishwa katika Bunge hilo na tume hiyo, zilionyesha kuwa pesa hizo zililipwa kwa walimu ambao ama wamekwishafariki dunia, wameacha kazi au walikuwa wakifanyakazi katika mwaka wa fedha 2021/2022.
Ripoti zinasema, Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC, Nancy Macharia, alikabiliwa na wakati mgumu kuieleza Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu (PAC) jinsi tume hiyo ilivyolipa kiasi hicho kikubwa cha pesa pasina kung’amua kuwa walimu hao hawakuwa kazini.
Dkt Macharia alikuwa amefika mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge Maalumu John Mbadi kujibu maswali yaliyoibuliwa kwenye ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Nancy Gathungu, kuhusu matumizi ya fedha katika TSC katika mwaka huo wa kifedha uliokamilika Juni 30, 2022.
Mbunge wa Soy, David Kiplagat amesema katika kikako cha kamati hiyo kwamba: “Nadhani ipo haja ya mifumo ya TSC ya ulipaji mishahara ifanyiwe ukaguzi wa kina. Naamini kuna hitilafu kubwa katika TSC. Isiposhughulikiwa inaweza kuzalisha sakata kubwa.”
Kwenye ripoti yake, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Kenya, Nancy Gathungu, alikuwa ameibua maswali kuhusu malipo ya pesa hizo Sh milioni 466.9, ambazo ni ongezeko la bajeti ya Shilingi milioni 352.9 katika mwaka huo wa fedha wa 2021/2022.