Kitaifa

SERIKALI YA QATAR YATOA MISAADA YA KIBINADAMU KWA WAATHIRIKA HANANG

Written by mzalendo

Balozi wa Qatar Nchini Tanzania Mhe. Fahad Rashed Almarekhi (wa pili kushoto) akikabidhi misaada ya kibinadamu kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga, ndani ya ndege iliyobeba misaada hiyo kwa ajili ya waathirika wa maafa ya maporomoko ya tope yaliyotokea tarehe 03 Disemba, 2023 katika Wilaya ya Hanang, Mkoa wa Manyara iliyopokelewa katika Uwanja wa ndege wa Kilimanjaro International Airport.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga (wa kwanza mbele), akishuka katika ndege iliyobeba misaada ya kibinadamu kwa ajili ya waathirika wa maafa ya maporomoko ya tope yaliyotokea tarehe 03 Disemba, 2023 katika Wilaya ya Hanang, Mkoa wa Manyara (anayefuata ni) Mkurugenzi Idara ya Mashariki ya Kati Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. BaloziAbdallah Kilima katika Uwanja wa ndege wa Kilimanjaro International Airport.

Balozi wa Qatar Nchini Tanzania Mhe. Fahad Rashed Almarekhi akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya makabidhiano ya misaada ya kibinadamu kutoka Nchini Qatar kwa ajili ya waathirika wa maafa ya maporomoko ya tope yaliyotokea tarehe 03 Disemba, 2023 katika Wilaya ya Hanang, Mkoa wa Manyara yaliyofanyika katika Uwanja wa ndege wa Kilimanjaro International Airport.

Picha ya pamoja ya baadhi ya viongozi wa Serikali, ujumbe wa Qatar na watendaji wengine baada ya makabidhiano ya misaada ya kibinadamu kutoka Nchini Qatar kwa ajili ya waathirika wa maafa ya maporomoko ya tope yaliyotokea tarehe 03 Disemba, 2023 katika Wilaya ya Hanang, Mkoa wa Manyara yaliyofanyika katika Uwanja wa ndege wa Kilimanjaro International Airport.
(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

Na Mwandishi wetu- Kilimanjaro

SERIKALI ya nchi ya Qatar imetoa msaada wa vyakula kwa ajili ya waathirika wa maafa ya maporomoko ya tope wilayani Hanang mkoani Manyara.

Akipokea msaada huo katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga alisema kuwa, misaada ya kibinadamu iliyotolewa na Qatar ni chakula kikavu katika vifungashio 1440, chakula kilicho tayari kuliwa katika vifungashio 3024 na vifaa vya usafi wa wanawake 4200.

Naibu Waziri huyo alisema kuwa, maporomoko hayo yalisababisha maafa katika Kata nne ambazo ni Gendabi, Ganana, Katesh na Jorodom na kusababisha madhara mbalimbali pamoja na vifo vya watu 89, majeruhi 139, nyumba 261 ziliathirika, mashamba ekari 754 ya wakulima 369 pamoja na Biashara 713.

“Serikali tunatambua mchango wa wadau wote ikiwemo wananchi, sekta binafsi asasi za kiraia na kidini, mashirika ya kimataifa na Umoja wa mataifa kwa ushiriki wao katika kusaidia wananchi walioathirika katika Wilaya ya Hanang.

Pia Serikali kwa kushirikiana na wadau na wananchi imeendelea kuchukua hatua kuhakikisha wananchi wa Hanang walioathirika wanarejea katika hali ya maisha ya awali,”Alisema Mhe. Ummy.

Naibu Waziri huyo aliongeza kuwa kwa sasa pamoja na kutoa misaada ya kibinadamu Serikali inaendelea na maandalizi ya ujenzi wa nyumba 108 za wananchi ambao nyumba zao zilibomoka kabisa au kuwa katika maeneo hatarishi katika eneo la Waret, Kijiji cha Gidagamond Kata ya Mogitu.

“Msaada huu utaenda kugusa maisha ya wananchi wa Hanang na Serikali inathamini ushiriki wa Wananchi wa Qatar na Serikali yake pamoja na taasisi ya misaada ya Qatar kupitia msaada wa kibinadamu ambao umetoa mchango mkubwa katika kuleta faraja, upendo na matumaini mapya kwa waathirika,”Alishukuru.

Kwa upande wake, Balozi wa nchi ya Qatar nchini Tanzania, Fahad Rashed Almarekhi alibainisha kwamba , Serikali ya Qatar imeamua kutoa msaada kwa Watanzania ambao wamekumbwa na maafa Hanang na utoaji wa msaada huo ni kielelezo cha kuthibitisha ukaribu na uhusiano mzuri uliopo baina ya nchi hizo mbili.

“Ujumbe wetu huu unaonyesha namna tulivyo na mashirikiano mazuri katika Nchi zetu hizi mbili, baada ya msaada huu tuma timu ya wataalam kuja kutambua mahitaji mengine ambayo hayakuguswa na msaada huu ili kutoa msaada mwingine ambao utakuwa ni suluhisho ya wananchi wa Hanang,”Alibainisha Mhe. Balozi Almarekhi.

Aidha Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga aliahidi kuhakikisha anasimamia vyema ugawaji wa misaada hiyo ili kuwafikia waathirika kama ilivyokusudiwa.
Ikumbukwe mnamo tarehe 03 Disemba, 2023 yalitokea maafa ya maporomoko ya tope yaliyoambatana na mawe, miti, magogo na maji kwa wingi kutoka Mlima Hanang kuelekea makazi ya watu.

About the author

mzalendo