KATIKA Mwaka wa fedha 2023/24 jumla ya Sh Bilioni 27.8 zimepelekwa kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya maji, vyoo bora na vifaa vya kunawia mikono kupitia mradi wa (WARSH) katika vituo vya kutolea huduma za afya 615 kote nchini vikiwemo vituo 28 katika Mkoa wa Mara vilivyopelekewa jumla ya Sh Bilioni 1.43.
Hayo yamesemwa leo bungeni katika kikao cha mwisho cha mkutano wa 14 wa Bunge 12 na Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Dkt Festo Dugange apokua akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Mhe Ghati Chomete.
Mbunge huyo alihoji mpango wa serikali wa kuhakikisha upatikanaji wa Dawa muhimu, X-Ray, Ultra Sound na maji ya uhakika kwenye Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali.
“ Serikali imeendelea kuboresha huduma za Afya zinazotolewa katika ngazi ya afya ya msingi. Katika mwaka wa fedha 2022/23 Serikali ilitoa jumla ya Sh Bilioni 66.7 kwa ajili ya kununua vifaa na vifaa tiba. Aidha katika mwaka wa fedha 2023/24 Serikali imetenga Sh Bilioni 117.3 kwa ajili ya kununulia vifaa na vifaa tiba katika ngazi ya afya ya msingi.
Hadi kufikia mwezi Januari 2024 jumla ya mashine za X-ray 407 na Ultra Sound 425 zilinunuliwa na kufungwa kote nchini ikiwemo X-ray 15 na Ultra sound 24 zilizofungwa katika vituo vya Mkoa wa Mara,” Amesema Mhe Dkt Dugange.
Amesema ili kuboresha usafi na upatikanaji wa maji vituoni, Serikali kupitia fedha za Benki ya Dunia na mapato ya ndani inatekeleza programu ya utoaji wa huduma za maji na usafi wa mazingira vijijini katika mikoa 25 ukiwemo mkoa wa Mara.